Thursday, 2 January 2014

Hofu ya bomu yazua taharuki


NA RABIA BAKARI
HALI ya taharuki jana iliwakumba wakazi wa eneo la Shekilango, jijini Dar es Salaam, baada ya kuona kitu aina ya chuma kilichokuwa kimejifukia ardhini na kuonekana sehemu ya juu, wakidhani kuwa ni bomu.
Taharuki hiyo ilizuka majira ya saa 3:00 asubuhi.
Hata hivyo, Polisi baada ya kupata taarifa, walifika katika eneo hilo na kukifukua kitu hicho na kuondoka nacho kwa ajili ya kukifanyia uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya uchunguzi wa awali kufanyika, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura, alisema wamegundua kwamba, kitu hicho si bomu na wala hakina kemikali yoyote inayoweza kuleta mlipuko.
“Kitu hiki (huku akikionyesha kwa waandishi wa habari), kinafanana na bomu, umbile na muonekano wake, lakini si bomu...ila tutaendelea kuchunguza ili kujua ni mabaki ya kitu gani, hivyo tunawatoa hofu wananchi kwamba wasiwe na wasiwasi,” alisema Kamanda Wambura.
Hata hivyo, alisema wamefarijika kuona mwamko wa wananchi wa kutoa taarifa pindi wanapohisi kitu cha hatari na kuwataka kuendelea kuwa makini.
“Tatizo ambalo bado lipo, ni kutochukua tahadhari, kwani baada ya kuhisi kwamba kuna bomu, wengi walisogelea eneo hilo, hali ambayo kama kweli kungekuwa na kitu cha mlipuko, kungetokea madhara makubwa.
Aliwatahadharisha watu kukaa mbalina eneo la tukio ili kuzuia kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Wambura, alisema, Polisi wamejipanga kuzuia uhalifu kwa kuongeza nguvu mara mbili ya kipindi cha sikukuu, na kuwataka wahalifu wakatafute eneo la kuishi.
“Kama hali ilivyoonekana wakati wa sikukuu, ndio itakuwa hivyo sikukuu zote na siku zote,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru