Sunday 5 January 2014

Mgeja awakomalia vigogo wa ujangili

Na mwandishi wetu, arusha

WIMBI la ujangili na usafirishaji wa nyara za serikali zikiwemo pembe za ndovu, hauwezi kukomeshwa iwapo vigogo wanaohusika na mtandao huo wataendelea kufichwa bila kuchukuliwa hatua.
Hatua hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuna baadhi ya watendaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi, hushiriki kwenye biashara ya pembe za ndovu, jambo linalosababisha tembo kuuawa kila kukicha.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Alisema hata wawekezaji wanaoingia nchini, wanapaswa kuchunguzwa kwani, wengine hujihusisha na biashara haramu ikiwemo ya pembe za ndovu.
Mgeja, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, alikuwa akitoa salamu za Mwaka Mpya wa 2014.
Alisema kwa muda mrefu sasa, baadhi ya watendaji serikalini na kwenye taasisi zake, wanatajwa kujihusisha na biashara hiyo.
Alisema hata katika taarifa ya Operesheni Tokomeza Ujangili iliyowasilishwa bungeni, baadhi ya watendaji wa serikali wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama, wabunge na wanasiasa, wametajwa kuhusika kwenye ujangili ikiwa ni pamoja na kuhujumu operesheni hiyo.

“Watendaji wa serikali wanatajwa katika ujangili na biashara haramu, tunatakiwa kuanza kuwashughulikia kwanza, ndipo baadaye twende kwa wadogo.
“Wananchi wanajitoa muhanga kuwataja, lakini serikali imekuwa na kigugumizi kuwachukulia hatua.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza, imewataja baadhi ya watendaji na wabunge kuwa walihusika kuihujumu kwa kuwa wako kwenye mtandao, tuchukue hatua kumaliza tatizo hili,’’ alisema Mgeja.
Alisema biashara ya pembe za ndovu mbali na kuteketeza wanyama kama tembo, lakini imeichafua Tanzania kimataifa, lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kukomesha.
Kufuatia hali hiyo, Mgeja alitoa wito kwa viongozi wa dini nchini, kuliombea taifa ili kuondokana na matukio mabaya yanayotokana na watendaji waliopewa dhamana kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Pia, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuanzisha madarasa maalumu kwa ajili ya mafunzo ya uzalendo hasa kwa vijana, yanayoendelea kwa sasa nchini ni matokeo ya kukosekana kwa uzalendo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru