Friday 3 January 2014

Wafuasi wa Zitto, CHADEMA wazichapa

NA FURAHA OMARY

WAFUASI wa CHADEMA na wale wanaodaiwa wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, jana walitwangana makonde nje ya viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hali hiyo ilijitokeza kabla na baada ya Jaji John Utamwa kusikiliza maombi ya Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, kuiomba mahakama itoe zuio la muda kwa Kamati Kuu ya chama hicho na chombo chochote kumjadili na kuamua kuhusu uanachama wake.
Vurugu hizo zilianza mapema saa 3.30 asubuhi, baada ya mahakama kutamka kwamba maombi ya Zitto ambayo amefungua dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA na Katibu Mkuu wa chama hicho, yatasikilizwa saa 4.30 asubuhi. Wafuasi wa chama hicho, ambao walikuwa wamefurika  walianza kumzomea Zitto, kwa madai ni fisadi na kwamba kesi aliyofungua inawapotezea muda.
Kutokana na hali hiyo, Zitto, aliyekuwa akilindwa na mabaunsa wawili na vijana wengine wawili, aliondoka eneo hilo na kwenda kukaa katika chumba maalumu kwa usalama wake.
Hali hiyo ilisababisha Wakili wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuwaita wanachama hao na kuwasihi watulie wasikilize walichoitiwa mahakamani hapo ili wasizuiwe kuingia mahakamani.
Hata hivyo, ilipotimia saa 5:50 asubuhi, wafuasi hao walianzisha fujo tena na kutaka kumpiga mtu mmoja kwa madai anawarekodi, jambo lililomlazimu mmoja wa askari kanzu kuingilia kati na kumuokoa mtu huyo.

Zitto amefungua kesi dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama hicho na Katibu Mkuu, Dk. Willbrod Slaa, akiiomba Mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu kujadili suala la uanachama wake hadi rufani yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Aidha anaomba Mahakama imwamuru Dk. Slaa ampe nakala za taarifa za vikao vilivyomvua uangozi ili akate rufaa.
Maombi ya Zitto, anayewakilishwa na Wakili Albert Msando, diwani wa CHADEMA, kata ya Mabogini, yalianza kusikilizwa saa 6.53 mchana, mbele ya Jaji John Utamwa.
Msando aliiomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Juzi Mahakama iliamuru Kamati Kuu kutojadili suala la uanachama wa Zitto katika Mkutano uliofanyika jana baada ya kutupilia mbali pingamizi la Chadema na kukubali ombi la Zitto.
Akiwasilisha hoja zake Wakili Msando aliomba zuio hilo litolewe hadi Zitto atakapopata nafasi ya kuwasilisha rufaa yake ya kupinga uamuzi wa kumvua uongozi katika Chama, uliotolewa katika kikao kilichofanyika Novemba 22, mwaka jana.

1 comments:

  1. hapo ndipo ukweli hujidhihilsha anakokata rufaa ni chadema.anao wapeleka mahakamani ni chadema.kisa nini madaraka.
    Zito hapo umechemsha.tungoje na kuona mwisho wako utakuwa vipi.
    huko Bungeni umechemsha kuwataja walioficha mabilioni Uswis.Au wamekwisha kugawia kitu kidogo.kutokuwataja hao umewasaidia CCM.hivyo adui yako amebaki mmoja tu naye ni Chama chako Chadema.ingawa CCC hujamalizana nao wanakusubiri Kigoma wakati wa Uchaguzi.vinginevyo ugombee ubunge kama mgombea wa CCM hapo watakulinda.vinginevyo kifo cha mende kinakungoja.

    ReplyDelete