Sunday 5 January 2014

Mama alilia haki ya kuishi na mwanaye

Na Rabia Bakari

MKAZI wa Kinondoni Dar es Salaam, Nuru Dominick, ameziomba taasisi za kisheria, kumsaidi ili kupata haki ya kuishi na mwanaye Abdurahim Abdul (2).
Abdul, kwa sasa anaishi na baba yake Abdallah Masoud, baada ya kutengana kutokana na sababu za kifamilia na kwamba, shauri hilo lilifikishwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Nuru alisema aliolewa na Masoud mwenye asilia ya Kiasia, lakini baadaye kulitokea ugomvi na hatimaye kutengana.
“Baada ya kutengena, akagoma kunipa mtoto na ameniwekea masharti magumu ambayo anajua kwa sasa sitayaweza...mtoto wangu ana miaka miwili, siko radhi awe mbali na uangilizi wangu,” alisema Nuru.
Alisema kesi hiyo ya mtoto imepita katika hatua mbalimbali kuanzia ya familia na hatimaye kupelekwa Baraza Kuu la Waislam Tanzania, ambako huko nako, waliamua mtoto aishi na baba yake bila kujali athari na umri alionao.
Alisema baada ya kuolewa mwaka 2009, Masoud alimbadili dini pamoja na kumuachisha kazi, lakini akiwa kwenye maisha ya ndoa, ndugu wa mumewe walimnyanyapaa hali iliyozua ugomvi, na hatimaye kuachana.
Alipotafutwa kuzungumzia madai hayo, Masoud alikiri kuishi na mtoto huyo na alisema hayuko tayari mwanaye alelewe katika mazingira mabovu na yasiyoridhisha.
“Hapa nyumbani nina mke na wafanyakazi, mtoto atalelewa, kinachomsumbua Nuru ni wivu, kuona mtoto analelewa na mama wa kambo, naelewa mtoto ni wetu sote na haki ya kukaa naye, lakini atafute mazingira mazuri kwanza, niridhike, ndipo nitampa mtoto,” alisema.
Hata hivyo, Nuru alisema Masoud alimwachisha kazi hivyo masharti anayompa ili kumrejesha mtoto huyo anatambua hataweza kuyatimiza na kuwa ni sehemu ya kuendelea kumnyanyasa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru