Friday, 28 June 2013

Amtoa roho mwenzake katika ulevi

Na Samson Chacha, Tarime

MKAZI wa kijiji cha Ngoreme, Maheli Chacha, anasakwa na Polisi kwa tuhuma za kumshambulia mwenzake na kumsababishia kifo.
Chacha, anadaiwa kumpiga marehemu huyo walipokuwa wakinywa pombe za kienyeji.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime /Rorya, Justus Kamugisha, alisema jana kuwa Chacha (43), anasakwa kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Kapecho Robert (41), mkazi wa kijiji cha Bisarwi, kata ya Nyangoto.
Alisema tukio hilo lilitokea Juni 26, mwaka huu, mchana, katika kijiji cha Bisarwi kata ya Nyangoto, baada ya kuzuka ugomvi kati ya mtuhumiwa na Robert.
Kamugisha alisema katika ugomvi huo, Maheli alimshambulia Robert kwa ngumi na mateke tumboni na kumsababishia maumivu makali ambapo alizimia na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya Tarime.
Alisema Robert alikufa siku iliyofuata wakati akipatiwa matibabu na mtuhumiwa alitoroka baada ya tukio.
Kamanda huyo, alisema polisi inaendelea kumsaka mtuhumiwa.
Pia, alisema mwili wa Robert umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo ukisubili kuchukuliwa na ndugu zake kwa mazishi.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mara watakapomwona Maheli ili aweze kuchukulia hatua za kisheria.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru