Wednesday, 19 June 2013

Vurugu zaathiri utalii Arusha
Na Waandishi Wetu, Arusha
SERIKALI imesema vurugu zilizofanywa mapema wiki hii zikihusisha viongozi na wafuasi wa CHADEMA mkoani hapa, zimeathiri taswira ya utalii nchini na kuyumbisha biashara kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu, aliyasema hayo jana jijini hapa alipozungumza na waandishi wa habari na kutoa msimamo wa wizara hiyo, kuhusiana na vurugu hizo pamoja na zile za Mei 5, mwaka huu, katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti.
“Nchi hivi sasa imeyumbishwa na matukio mawili, jambo ambalo linawafanya watalii pamoja na wafanya biashara kushindwa kufanya shughuli zao kama kawaida,” alisema Nyalandu.
Kufuatia matukio hayo, Nyalandu alisema serikali itawachukulia hatua kali za kisheria wale wote walioshiriki katika tukio la ulipuaji wa bomu ambao inadaiwa wamenunuliwa ili wawaue na kuwajeruhi watu wasio na hatia.
“Sote tunajua kuwa tukio la Mei 5, mwaka huu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiti, lilisababisha pia kuyumba kwa biashara na uingiaji wa watalii nchini.
“Lakini tukiwa tunaendelea kulitafakari hilo, hili nalo linatokea. Sasa hali hii inachangia kuathiri uingiaji wa watalii nchini na kusababisha wafanyabiashara nao kushindwa kuendelea na shughuli zao kama ilivyokuwa imezoeleka,”alisema Nyalandu.

Alisema endapo hali ya utulivu haitatengamaa, wafanyabiashara watashindwa kufanya kazi kwa uhuru pamoja na watalii kushindwa kutembelea mbuga za wanyama na vivutio vingine vya utalii.
Kwa mujibu wa Nyalandu, Tanzania kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupokea watalii milioni moja kwa kipindi cha mwaka jana, Kenya wakiwa wanaongoza kwa kuwapokea milioni mbili hadi tatu.
Hata hivyo, alisema matukio kama hayo yanafifisha juhudi za serikali za kuendelea kuutangaza utalii.
Alisema tayari nchi ya Italia imeshaahirisha safari za kitalii ambapo watalii wengi toka nchini humo hutembela kwa wingi visiwa vya Zanzibar.
Aidha, alisema mwaka jana zaidi ya watalii milioni 2.4 walitembelea katika hifadhi za taifa.
Nyalandu alihadharisha kuwa, endapo matukio yenye sura ya kigaidi yataendelea kutokea nchini, mapto ya utalii yatashuka kwa asilimia kubwa na hivyo, kuathiri uchumi wa nchi.
Wakati huo huo, Naibu waziri huyo alisema  ziara ya Rais Barrack Obama ipo pale pale na atatembelea moja ya hifadhi za taifa ambayo hakuitaja.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru