Wednesday, 26 June 2013

TRA yaboresha mtandao wa kodi


Na Hamis Shimye
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya imeboresha ulipaji kodi kwa njia ya mtandao kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi.
Uboreshaji huo ni pamoja na kuzindua mtandao utakaosaidia kupatikana kwa taarifa za kodi kwa wananchi na kuunganisha kwa mawasiliano baina ya TRA na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akizungumza jana na waandishi wa habari kuhusiana na uboreshaji huo, Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Salehe Mshoro, alisema utasaidia pia mifumo ya kompyuta ya BoT na TRA kuungana.
Mshoro alisema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi mengine katika ulipaji wa kodi, ambapo mfumo huo utaanza kutumika Julai Mosi, mwaka huu kwa wafanyabiashara wakubwa na baadae kwa wafanyabiashara wengine nchini.
Naye, Meneja Mradi huo unaojulikana kana  ‘Revenue Gateway’, Ramadhan Singati, alisema umebuniwa na TRA kwa kushirikiana na BoT.
Alisema nia ni kuongeza uwezo katika ukusanyaji wa taarifa na ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara.
“Hautakuwa na matatizo hata kidogo, kwani ni mfumo bora na una uwezo mkubwa kutokana na aina ya teknolojia iliyopo na ni salama kwa fedha na taarifa,” alisema Singati.
Kwa upande wake, Kamishina wa Upelelezi wa Kodi wa TRA, Lusekelo Mwaseba, alisema wamejipanga kikamilifu na wana vifaa na rasilimali watu ya kutosha kuendesha mitambo hiyo na hakuna hujuma itakayojitokeza.
Alisema mfumo huo ni mzuri na utakuwa na faida kubwa kwa wateja na pia, utasaidia kuwaondolea usumbufu katika ulipaji kodi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru