Wednesday, 26 June 2013

Jalada la Sugu latinga kwa DPP


Na Mwandishi Wetu, Dodoma
POLISI mkoani Dodoma imekamilisha upelelezi wa tuhuma zinazomkabili mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu (CHADEMA), anayetuhumiwa kumtukana Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kupitia mtandao wa kijamii.
Imeelezwa jalada limepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua zaidi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, David Misime, alisema jana kuwa, polisi imeshakamilisha upelelezi wa tuhuma hizo na jalada kupelekwa kwa DPP.
“Polisi tumeshakamilisha upelelezi na jalada liko kwa DPP kwa hatua zaidi kwa jinsi atakavyoona inafaa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Sugu jana aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi kama alivyotakiwa kufanya na kwamba, ameongezewa dhamana hadi leo, ambapo anatakiwa kuripoti kituoni.
“Jana alitimiza masharti ya dhamana kwa kuja kuripoti, anaendelea na dhamana hadi kesho, tukisubiri uamuzi wa DPP,” alisema.
Sugu alikamatwa juzi, saa nane mchana, akitoka bungeni, akituhumiwa kumtukana Pinda kwa kutumia mtandao wa kijamii.
Kwa mujibu wa Misime, baada ya kukamatwa, Sugu alifikishwa Kituo Kikuu cha Polisi alikohojiwa kwa takriban saa mbili na nusu.
Mbunge huyo anatuhumiwa kumtukana Waziri Mkuu Pinda kuhusu utendaji wake wa kazi na kumdhalilisha.
Anatuhumiwa kumtusi waziri mkuu kutokana na kauli aliyoitoa hivi karibuni bungeni alipojibu maswali ya papo kwa hapo.
Waziri Mkuu Pinda alivitaka vyombo vya dola, likiwemo Jeshi la Polisi kutowavumilia watu wanaotishia amani na utulivu nchini.
Sugu amedhaminiwa na mbunge mwenzake wa CHADEMA, Tundu Lissu na mtu mwingine, mkazi wa Dodoma.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru