Vijiji Mikumi kupata umeme
VIJIJI saba vya jimbo la Mikumi, mkoani Morogoro, vinatarajiwa kupatiwa umeme wa gridi ya taifa katika mwaka ujao wa fedha.
Akijibu swali la Abdulsalaam Ameir (Mikumi -CCM), Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), linafanya tathmini ili kubaini gharama halisi.
Simbachawene alivitaja vijiji hivyo kuwa, Zoumbe, Lumbe, Kipekenya, Ulaya Mbuyuni, Ulaya Kibaoni, Nakala na Mhenda.
Ameir alitaka kujua ni lini serikali itapeleka umeme katika vijiji hivyo, ili viweze kutumia nishati hiyo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa Simbachawene, baada ya tathmini serikali itatafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, ikiwemo Mfuko wa Nishati Vijijini.
Hata hivyo, katika swali la nyongeza la Yussuf Nasir (Korogwe Mjini -CCM), aliyetaka kujua kama azma hiyo itatimizwa kwa kuwa vijiji hivyo haviko kwenye awamu ya pili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA), naibu waziri alisema vitaingizwa katika awamu ya tatu.
Alisema baada ya awamu ya pili, REA inatarajiwa kuanzisha awamu ya tatu, ambayo itajumuisha vijiji vingine, vikiwemo vilivyotajwa na Malolo na Malolo Wasaganza katika jimbo hilo.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru