Tuesday, 25 June 2013

Mitihani TEKU kutokufanyika


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA

UMOJA wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKUASA), umesema hautatoa mitihani kwa wanafunzi inayotarajia kuanza Jumatatu ijayo, iwapo uongozi wa chuo hautayafanyia kazi madai yao.
Imeelezwa licha ya TEKUASA kuandika barua ya malalamiko kuhusu madai yanayotishia kuporomoka taaluma chuoni hapo, uongozi wa TEKU haujarudisha majibu kwa maandishi.
Kaimu Mwenyekiti wa TEKUASA, Aman Simbeye, alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliohudhuriwa na wahadhiri wa chuo hicho.
Simbeye akizungumza chuoni hapo, alisema utaratibu wa uendeshaji wa elimu ya juu chuoni hapo unatia shaka.
Alisema licha ya TEKUASA  kuandika barua kwa menejimenti ya chuo ili kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali, hakuna majibu waliyopatiwa.
Kwa mujibu wa Simbeye, wanafunzi walioghushi vyeti na kufukuzwa wamerejeshwa chuoni kinyemela, kitendo ambacho hawakiafiki.
“Sisi ni jicho na mfano kwa jamii, kamwe hatuwezi kukubali kuona mambo yanaendeshwa kienyeji chuoni hapa, kwani mwisho wa siku chuo kitatoa wanafunzi wasio na sifa na lawama zitaturudia,” alisema.
Alisema wapo wahadhiri waliokwenda kuongeza elimu na wamewasilisha vyeti, lakini uongozi wa TEKU hautaki kuwapandisha madaraja, huku wengine wakishushwa na stahili walizokuwa wakipata zimeondolewa.
Mhadhiri huyo alisema wanashangazwa na uamuzi unaofanywa na menejimenti ya chuo, kwa kuwapandisha vyeo wahadhiri wengine, huku baadhi wakikataliwa.
Kwa mujibu wa Simbeye, kuna wahadhiri wasio na sifa, lakini wameajiriwa, jambo linaloshusha ari ya utendaji wa wahadhiri wengine.
Alisema chuo hicho kwa muda mrefu hakina kitengo cha kusimamia ubora wa elimu inayotolewa, hivyo iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa na serikali, wanaohitimu hawatakuwa na sifa zinazostahili kitaaluma.
Simbeye alisema kuna mwanafunzi ambaye alitakiwa kurudia kozi lakini hakufanya hivyo, na katika hali ya kushangaza amepewa daraja ambalo hakustahili.
Alisema chuo hicho hakina chombo cha kupitisha matokeo ya wanafunzi baada ya kupitiwa na wahadhiri. Kutokana na hilo, alisema matokeo yaliyotangazwa ni batili.
Simbeye alisema jengo la maabara limejengwa chini ya kiwango, hivyo kuwa na nyufa nyingi na halifai kwa matumizi.
“Utawala umekuwa unatumia lugha za vitisho na matusi, kila tunapotaka kupata ufafanuzi wa jambo lolote, hali ambayo inavunja ari ya utendaji,” alisema.
Makamu Mkuu wa chuo, Profesa Tully Kasimoto hakupatikana kuzungumzia madai hayo ya wahadhiri. Ilielezwa kuwa yuko Dar es Salaam.
Kaimu Makamu Mkuu wa TEKU, Dk. Daniel Mosses, alisema si msemaji wa chuo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru