Wednesday, 26 June 2013

Mke aua mumewe kwa kumsukuma


NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MKAZI wa kijiji cha Iganduka, kilichopo wilayani Mbozi, amekufa baada ya kusukumwa na mke wake na kuangukia kisogo.
Inadaiwa alikuwa na ugomvi na mkewe huyo.
Ugomvi huo unadaiwa kuzuka baada ya mkazi huyo, aliyetajwa kwa jina la Rodrick Mwaipasi (55), kumtuhumu mkewe kuuza madebe mawili ya Karanga, bila ya idhini yake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, alisema tukio hilo lilitokea Juni 24, mwaka huu saa 4:00 usiku, katika hospitali ya misheni Mbozi, ambapo marehemu alipelekwe kupatiwa matibabu.
Athuman alisema mzozo huo wa kifamilia ulizuka baada ya mke wa marehemu, aliyemtaja kuwa Makrina Mateo (42) maarufu kwa jina la Simbowe, kuuza debe hizo za Karanga huku mumewe akiwa hana taarifa.
“Hivyo kulitokea mzozo wa kifamilia baina ya wanandoa hao wawili, ambapo Makrina alimsukuma mumewe ambaye aliangukia kisogo,” alisema Kamanda Athuman.
 Alisema Polisi walifanikiwa kumtia mbaroni mke huyo wa marehemu na utaratibu unafanywa ili aweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma.
Kamanda Athuman, alitoa wito kwa jamii kutatua matatizo ama migogoro yao kwa njia ya mazungumzo, badala ya kujichukulia sheria mkononi kwa kutumia hasira na nguvu.
Katika tukio lingine, dereva mmoja amekufa papo hapo na abiria wake kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupasuka gurudumu la mbele upande wa kushoto na kupinduka.
Athuman alisema ajali hiyo ilitokea Juni 25, mwaka huu saa 2:00 asubihi, katika kijiji cha Urunda wilayani Mbarali, ambapo ilihusisha gari lenye namba ya usajili T.545 AUL aina ya Toyota Escudo.
Alimtaja dereva aliyekuwa anaendesha gari hilo kuwa ni Abinery Chaula (45), mkazi wa Mkombwe – Ubaruku, wilayani humo.
Alisema kufuatia ajali hiyo, dereva alikufa papo hapo na abiria aliyekuwemo ndani ya gari hilo, Johari Uguda (37), anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya misheni Rujewa.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo na uchunguzi zaidi kuhusiana na ajali hiyo unaendelea.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru