NA RABIA BAKARI
JESHI la Polisi limeimarisha ulinzi mara dufu, kutokana na ujio wa wakuu wa nchi zaidi ya 14, walioanza kuingia nchini jana.
Miongoni mwa wakuu hao wa nchi ni Rais wa Marekani, Barack Obama, atakayewasili Jumatatu.
Jeshi hilo pia limepiga marufuku maandamano ya CUF na mengine yaliyoandaliwa kwa siri, yakilenga kusambaza vipeperushi na mabango wakati Rais Obama atakapowasili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema wana taarifa za uhakika kuwa, kuna chama cha siasa na taasisi ambazo zimejiandaa kujitokeza na mabango, kitendo ambacho ni kinyume cha utaratibu wa usalama.
“Uchunguzi wa hali ya juu unafanyika kuwabaini wahusika. Hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayeleta vurugu wakati wa ugeni huo. Tunawasihi kuwa watiifu wa sheria bila shuruti,” alionya.
Kuhusu maandamano ya CUF, alisema yalilenga kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete. Alisema wamekwisha kujibiwa na Ikulu kwamba, rais hataweza kuonana au kupokea maandamano hayo, kwa kuwa atakuwa na ugeni.
“Maandamano hayo pia yataingilia misafara ya viongozi na wajumbe wao. Barabara wanayotarajia kutumia ipo katika orodha ya zitakazotumika wakati wa ugeni huo mkubwa,” alisema.
Akizungumzia ulinzi, alisema polisi wengi watakuwa barabarani na mitaani na kwamba, jambo hilo ni la kawaida katika kuimarisha usalama kwa kipindi hicho, hivyo wananchi wasiwe na hofu.
“Licha ya ujio wa Obama, tuna wageni mbalimbali watakaoshiriki mkutano wa Smart Partnership utakaoanza keshokutwa.
“Mkutano huu ni wenye manufaa kwa nchi. Tukiachana na upolisi au uandishi wa habari, wote tuungane na kuwa wazalendo kwa matokeo mazuri ya mkutano huo,” alisema.
Alisema baadhi ya nchi zimetuma vikosi vya usalama ambavyo vinashirikiana na jeshi hilo. Alisema ikilazimika watatumia helikopta kuhakikisha amani haivurugiki.
Kova amewaomba wamiliki wa hoteli na magari binafsi au ya umma kuwa waaminifu na wazalendo ili kutangaza sifa nzuri ya taifa. Wametakiwa kulinda mali za wateja wanaotumia huduma zao.
Alisema wanaangalia uwezekano wa kuondoa usumbufu, hususan katika matumizi ya barabara, lakini wananchi wanatakiwa wawe wavumilivu, kwani mahitaji yatakuwa makubwa.
Kamanda Kova alisema elimu ya matumizi ya barabara itatolewa na kila linalowezekana litafanyika ili kuhakikisha matumizi ya barabara hayaleti adha kwa watumiaji.
Alisema wasiokuwa na mambo muhimu ya kufanya mjini, ni vyema wawe watulivu majumbani.
Wednesday, 26 June 2013
Ulinzi mkali ujio wa Rais Obama
09:54
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru