Tuesday, 25 June 2013

Wafanyakazi 15 TRA wachunguzwa

Na Epson Luhwago, Dodoma
BUNGE limepitisha bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/2014, ambayo itatumia sh. trilioni 18.2 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. 
Bajeti hiyo ilipitishwa jana kwa wabunge kupiga kura kukubali au kuikataa. Jumla ya wabunge 270 walikuwepo wakati wa kupiga kura, ambapo kura za NDIYO zilikuwa 235 na za HAPANA 35.
Wabunge wote wa CCM waliokuwepo waliikubali, huku wapinzani wakiikataa. CHADEMA hawakupiga kura kwa madai hawakushiriki kuijadili.
Hata hivyo, mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), kama ilivyo ada, aliikubali. Alisema anaiunga mkono tangu alipokuwa akiijadili. Kila mwaka amekuwa akiunga mkono bajeti ya serikali.
Licha ya upigaji kura ambao ni hatua ya mwisho, wabunge walijadili kwa siku nne mfululizo na kutoa hoja mbalimbali. Wabunge 119 walichangia kwa kusema na wengine 36 kwa maandishi.
Awali, akijibu hoja za wabunge waliochangia, Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, alisema bajeti iliyopitishwa imekidhi vigezo na kujibu maswali muhimu ambayo wataalamu wa bajeti wanataka yazingatiwe.  Vigezo hivyo, kwa mujibu wa Waziri Mgimwa ni kuleta unafuu kwa wananchi, kiwango cha upunguzaji umasikini, kutambua umuhimu wa makundi yaliyosetwa kama wanawake na vijana, na kutambua vipaumbele muhimu.
“Bajeti hii imekidhi mambo hayo muhimu kwa sababu imetoa majibu kwa kuweka kipaumbele kwenye uwekezaji wa mambo muhimu ya kiuchumi. Mfano ni kutengwa kwa sh. trilioni 1.2 kwa ajili ya miundombinu ya barabara, umeme na usafirishaji ili kuchochea uzalishaji nchini,” alisema.
Katika kudhihirisha bajeti inajali maisha ya wananchi, Dk. Mgimwa alisema serikali imejikita katika kutatua kero za maji, umeme, pembejeo za kilimo na umeme vijijini.
Alisema umeme vijijini pekee umetengewa sh. bilioni 186 ili kuwawezesha wananchi wa maeneo hayo yapate nishati hiyo na maji yametengewa sh. bilioni 184.5.
Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele kwa kuongezewa bajeti na kiasi katika mabano ni uwekezaji maeneo maalumu -EPZ (sh. bilioni 30), usafirishaji (sh. bilioni 30), mifugo (sh. bilioni 20) na mfuko wa mbolea (sh. bilioni 21.5).
Kuhusu hoja ya kukusanya kodi kutoka kampuni za madini, alisema zimekuwa zikikusanywa na juhudi zinafanywa ili kuzibana ziweze kulipa kodi zaidi kutokana na fedha zinazopata.
Alisema kampuni hizo zimekuwa zikilipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kampuni, maendeleo ya elimu, ushuru wa stempu na kodi za mapato.
Dk. Mgimwa alitoa takwimu za kodi zinazolipwa kwa miaka mitano katika mabano kuwa, 2007/08 (sh. bilioni 69.5), mwaka 2009/10 (sh. bilioni 66.6), 2010/11 (sh. bilioni 85.5), 2011/11 (sh. bilioni 119), 2011/2012 (sh. bilioni 274.8) na kwa mwaka 2012/13 hadi kufikia Machi mwaka huu zilikusanywa sh. bilioni 251.8.
“Kwa miaka yote hiyo mitano, serikali imekusanya sh. bilioni 867.38 kutoka kwa kampuni za Bulyanhulu, North Mara, Pangea, Resolute, Tanzanite One na Williamson Diamond,” alisema. 
Kwa kampuni zinazofanya utafiti na utafutaji wa mafuta na gesi, alisema haziwezi kutozwa kodi kwa kuwa hazijaingizwa katika utaratibu huo, kwani hazijaanza kuzalisha.
Hata  hivyo, Dk. Mgimwa aliwaondoa hofu juu ya kasi ya kupungua kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 19.8 hadi asilimia 8.4 kwa kusema ni takwimu ni za kweli.
Alisema hatua hiyo imetokana na kudhibiti uhaba wa chakula na mafuta, ambavyo ndivyo chanzo kikuu cha kupanda kwa mfumuko wa bei. Pia alisema hatua hiyo ilitokana na kupunguzwa kwa ushuru wa bidhaa za mafuta na kuwabana waliokuwa wakichakachua.
Waziri alisema kodi ya mapato kwa wafanyakazi iliyopendekezwa kupunguzwa hadi asilimia 10 kutoka asilimia 13 iliyopendekezwa na serikali itabaki kama ilivyo. Aliahidi kuwa kodi hiyo itapunguzwa mwaka hadi mwaka.
Katika harakati za kupunguza matumizi makubwa yasiyo na tija,  alisema serikali imekubali hoja za wabunge na kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha magari yatanunuliwa kwa mfumo wa jumla. Pia alisema serikali itapunguza misamaha ya kodi kwa maeneo yasiyo na tija.
Alisema serikali inakusudia kubadilisha sheria ya ununuzi wa umma ili kuwabana wanaonufaika na mfumo wa sasa na kuigharimu serikali fedha nyingi katika eneo hilo.

WAFUTWA KAZI TRA
Katika hatua nyingine, wafanyakazi 15 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamefukuzwa kazi katika miaka mitatu iliyopita kwa kujihusisha na njama za kuikosesha serikali mapato.
Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, alisema hayo bungeni jana, alipojibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya serikali ya mwaka 2013/2014.
Alisema wafanyakazi hao walifukuzwa kazi kutokana na  kushirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi, hivyo kuifanya serikali kukosa mapato yanayostahili.
Kwa mujibu wa Janet, wafanyakazi hao wamefukuzwa kazi kati ya mwaka 2010 na Mei, mwaka huu, katika sehemu mbalimbali ikiwemo, Dar es Salaam.
Kuhusu kuhamishwa kwa maofisa waliotuhumiwa kuhusika na wizi wa makontena bandarini, alisema hatua hiyo imefanyika ili kutoa nafasi kwa uchunguzi unaoendelea.
“Huo ni utaratibu wa kawaida wa TRA kwa kuwa huwezi kumwacha mtuhumiwa katika kituo chake cha kazi wakati uchunguzi unafanyika. Baada ya kukamilika uchunguzi hatua zinazostahili kwa mujibu wa sheria zitachukuliwa,” alisema.
Naibu waziri alisema utoroshaji wa makontena bandarini, ulifanywa na maofisa wa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na mawakala wa forodha wasio waaminifu. Alisema mawakala hao watachukuliwa hatua kulingana na ripoti ya uchunguzi itakayotolewa.
Alikiri rushwa imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa serikali kukosa mapato ndani ya TRA na kutokana na hilo, mamlaka imeanzisha mkakati wa kupambana na rushwa, ambao umesaidia kubaini wahusika na kuwachukulia hatua.
Ili kuhakikisha wafanyakazi wanaoajiriwa wanakuwa waadilifu, alisema hivi sasa TRA imekuwa ikiwafanyia uchunguzi kupitia vyombo mbalimbali vya usalama ndani na nje ya mamlaka. 
MADUKA YAFUTIWA LESENI
Wakati huo huo, maduka 17 ya kubadilishia fedha yamefutiwa leseni kutokana na kukiuka sheria na masharti ya uendeshaji wa shughuli, imefahamika.
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema bungeni jana kuwa, maduka hayo yamechukuliwa hatua baada ya kubainika yalikuwa yakiendesha shughuli kinyume cha utaratibu.
Alisema maduka mengine matano yamefungiwa kwa muda, 33 yametozwa faini na mengine 103 yamepewa onyo kali kutokana na makosa yaliyofanywa kutokuwa makubwa.
Saada alisema hatua hiyo iliyochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo ndiyo msimamizi wa maduka hayo, kwa mujibu wa Sheria ya Kubadilisha Fedha.
Alisema moja ya makosa yaliyofanywa na maduka hayo ni kutokufanya biashara inayozidi dola 10,000 (zaidi ya sh. milioni 160) kwa siku kwa duka moja.
“Hiki ndicho kiwango cha juu kwa bureau de change (duka la kubadilisha fedha). Kiasi kinachozidi hapo ni lazima kiombewe kibali, vinginevyo hatua zinaweza kuchukuliwa,” alisema.
Alisema kwa sasa, ili maduka hayo yaweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, masharti makali yamewekwa, ikiwemo ya kusajiliwa kama kampuni.
Sharti la pili kwa mujibu wa Saada ni wamiliki lazima wawe Watanzania na la tatu ni kutofanya biashara nyingine nje ya kubalisha fedha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru