Wednesday, 26 June 2013

Utekelezaji wa miradi wamleta Obama nchini


Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema moja ya sababu ya Rais wa Marekani Barack Obama kufanya ziara nchini ni kutokana na kuvutiwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utawala wa kidemokrasia.
Pia, imesema amelenga kujionea matumizi mazuri ya fedha za misaada zinazotolewa na nchi yake kwa ajili ya kuboresha maendeleo katika sekta mbalimbali nchini, zikiwemo za miundombinu, afya na elimu.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Kituo cha Radio Clauds cha jijini Dar es Salaam.
Membe, alisema Rais Obama anakuja nchini kutokana na kuvutiwa na serikali inavyotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia utawala bora na demokrasia, jambo ambalo ni tofauti na mataifa mengine.
Alisema nchi nyingi duniani zinaiangalia Tanzania kama taifa lililopiga hatua katika vigezo vya amani duniani, ukilinganisha na mataifa mengine.
Alisema Tanzania inatumia muda mwingi kushughulikia migogoro ya uvunjifu wa amani katika nchi jirani.
Kwa mujibu wa Membe, licha ya baadhi ya watu kudharau utendendaji wa serikali katika kusimamia utawala wa kidemokrasia, mataifa mbalimbali duniani yanaiangalia kama taifa lililopiga hatua katika Nyanja ya utawala wa kidemokrasia.
Membe alisema katika nchi 54 barani Afrika, Tanzania imepiga hatua kubwa katika vigezo vya amani.
Alisema kidunia inashika nafasi ya 55 ns imeendelea kufuata falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo.
Alisema hata Rais wa China Xi Jinping aliahidi kuitembelea Tanzania kabla ya kuchaguliwa kuwa rais na alitekeleza ahadi hiyo.
Alisema ziara yake ilikuwa na manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi kwani  alisaini mikataba 18 ya maendeleo pamoja na kutangaza sera ya uchumi ya China na muelekeo wa uhusiano wake na nchi za Afrika.
Wakati huo huo; Waziri Membe amewashauri wananchi kutumia mkutano huo kama fursa ya kujiongezea kipato, hususani kwa wajasiriamali.
Amewataka watafute maeneo na kufanya biashara kama ya vyakula, kwakuwa wageni wanaokuja nchini ni wengi na tayari hoteli na migahawa imeshajaa.
“Na wengine watataka hata kula vyaula vyetu vya asili na kununua vitu mbalimbali, kwa hiyo wajasiriamali wajipange,” alisema Membe.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru