NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya Kikwete amemteua Luteni Kanali Lidwino Mgumba, kuwa Naibu Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isaac Nantanga, uteuzi huo ulianza Juni 20, mwaka huu.
Taarifa hiyo, ilisema kuwa Luteni Kanali Mgumba ambaye ni Ofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ni mchambuzi na mtaalamu wa kijeshi katika masuala ya ulinzi, amani, diplomasia, usuluhishi wa migogoro na mawasiliano ya umma.
Ilisema kuwa taaluma hizo alizipata katika vyuo mbalimbali vikiwemo vya kijeshi na vya kiraia ndani na nje ya nchi.
Pia, ilisema Luteni Kanali Mgumba amewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika JWTZ ikiwemo Msaidizi wa Kijeshi wa Mkuu wa Komandi ya Jeshi la Nchi Kavu na kuwa Msaidizi wa Kijeshi wa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru