Tuesday, 25 June 2013

KUTOKA BUNGENI DODOMA LEO


SIMU ZISIZOSAJILIWA MWISHO JULAI 10
SERIKALI inatarajia kuzima simu zote za mkononi ambazo hazijasajiliwa Julai 10, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema hayo jana, alipojibu swali la Dk. Getrude Rwakatare (Viti Maalumu -CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya serikali kuhusu baadhi ya watu ambao wanatumia simu za mkononi kusambaza ujumbe wa uzushi kwa wengine.
January alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya serikali katika kudhibiti matumizi mabaya ya simu za mkononi.
Alisema serikali imeondoa muda wa siku 30 zilizowekwa kwa ajili ya mnunuzi kutumia simu kabla ya kusajiliwa.
Naibu waziri alisema namba za simu 24,4036,999 zimesajiliwa na serikali.
Kwa mujibu wa January, usajili wa simu unalenga kupunguza matumizi mabaya yaliyoanza kujitokeza.
Alisema licha ya kuzisajili, serikali imekumbana na changamoto mbalimbali za matumizi mabaya ya simu.
Baadhi ya changamoto hizo alisema ni mawakala kusajili simu bila kutumia vitambulisho au majina halisi ya watumiaji.

HALMASHAURI ZAONYWA MADENI YA WALIMU
OFISI ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, imetoa maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri kutosababisha madeni ya walimu.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Kassim Majaliwa, alitoa maelekezo hayo alipojibu swali la Meshack Opolukwa (Meatu -CHADEMA).
Opolukwa alitaka kujua ni lini serikali itaondoa tatizo la walimu Meatu la kuchelewesha kupandishwa madaraja na kutolipwa stahili zao.
Majaliwa alisema serikali imedhamiria kuondoa tatizo la walimu kuchelewa kupandishwa madaraja na kulipwa stahili zao, ikiwa ni pamoja na kuimarisha na kuboresha mfumo wa taarifa za watumishi.
Alisema ili kuepuka madeni, halmashauri zimetakiwa kutenga fedha za kuwapandisha madaraja watumishi, wakiwemo walimu na kuhakikisha marekebisho ya mishahara yanalipwa kwa wakati.
Naibu waziri alisema katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 serikali imetenga nafasi za kuwapandisha vyeo walimu 39,602 walio katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na kwamba, sh. milioni 64 zimetengwa.
Majaliwa alisema fedha hizo zimetengwa kupandisha madaraja walimu 330 wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu.
Katika mfumo huo, alisema serikali inaweka utaratibu wa kiutumishi wa kushughulikia malimbikizo ya mishahara, uhamisho, ukomo wa watumishi na marekebisho ya taarifa za mtumishi.
Alisema serikali imeunda kamati ya kuchambua na kutoa mwongozo kwa ajili ya kushughulikia changamoto ya upandishwaji madaraja walimu.
Kamati hiyo alisema itawasilisha  mapendekezo katika Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika sekta ya elimu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru