Wednesday, 19 June 2013

Simba huru kesi ya UDA


Na mwandishi wetu
MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, amewasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea
kuwashitaki Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la UDA, Idd Simba na wenzake.
Simba, aliyewahi kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi wa shirika hilo, Salim Mwaking'inda,
Meneja Mkuu wa UDA, Victor Milanzi na Mkurugenzi wa Kampuni ya Simon Group Ltd, Simon Kisena, walikuwa wakishitakiwa kwa shitaka la uhujumu uchumi.
Kutokana na hatua hiyo ya DPP, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mugeta,
aliifuta kesi ya uhujumu uchumi namba 3/2013, iliyokuwa ikiwakabili washitakiwa hao.
Awali, Wakili wa Serikali Awamu Mbagwa, alidai kesi hiyo ilipagwa jana ili upande wa Jamhuri uwasomee
maelezo ya awali washitakiwa, lakini kutokana na hati ya DPP ya kutokuwa tayari kuendelea na
kesi dhidi ya washitakiwa hawawezi kufanya hivyo.
Wakili Alex Mgongolwa, anayemtetea Simba, alidai upande wa utetezi hauna pingamizi kuhusu hati hiyo,
lakini upande wa Jamhuri usiwasumbue tena wateja wao.
Hakimu Mugeta alisema kwa kuwa kesi hiyo ni ya jinai iliyofunguliwa na Jamhuri na imewasilisha hati ya
kutokuendelea kuwashitaki washitakiwa, mahakama haina mamlaka ya kupingana na hati hiyo.
“Kutokana na hilo, nawafutia kesi hiyo ya uhujumu uchumi  washitakiwa wote,” alisema.
Upande wa Jamhuri Aprili 30, mwaka huu, uliifuta kesi ya awali, ambayo walishitakiwa kwa matumizi
mabaya ya madaraka.
Kesi hiyo ilikuwa ikimkabili Simba, Mwaking'inda na Milanzi. 
Baadaye ilifungua kesi mpya, washitakiwa wakikabiliwa na mashitaka sita, yakiwemo ya rushwa na
uhujumu uchumi, ambapo Kisena aliunganishwa.
Katika shitaka la kwanza la kula njama, Simba, Milanzi na Kisena walikuwa wakidaiwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, jijini Dar es Salaam, walikula njama za kutenda kosa la vitendo vya rushwa.
Kisena katika shitaka la pili alidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa. Hata hivyo, halikusomwa
kutokana na mshitakiwa kutokuwepo mahakamani.
Shitaka la tatu liliwahusu Simba na Milanzi waliodaiwa kati ya Septemba 2009 na Januari 2010, walipokea sh. milioni 320 kutoka kwa Kisena, zikiwa ni ushawishi wa kuiuzia Simon Group hisa za UDA, ambazo zilikuwa hazijagawiwa.
Simba, Mwaking’inda na Milanzi katika shitaka la nne, walishitakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru