ANGA la Tanzania litafungwa kwa nusu saa kabla ya kuwasili ndege ya Rais Barack Obama wa Marekani, Jumatatu mchana.
Rais Obama anatarajiwa kuwasili nchini akitoka Afrika Kusini, baada ya kuzuru Senegal, katika ziara yake ya pili barani Afrika, tangu aingie madarakani.
Ujio wa Rais Obama unasubiriwa kwa hamu, huku wengi wakiwa na matarajio ya kuboreshwa au kuongezwa ufadhili wa miradi ya maendeleo.
Kutokana na ujio wa Obama, ambaye ni kiongozi wa taifa kubwa duniani, ulinzi umeimarishwa katika maeneo mbalimbali nchini, hususan Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na hoteli kadhaa za Jiji la Dar es Salaam, ambazo ujumbe wa kiongozi huyo utafikia.
Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Deusdedit Kato, akizungumza na gazeti hili jana, alisema maandalizi yamekamilika na ulinzi umeimarishwa.
Alisema anga la Tanzania litafungwa kwa nusu saa kabla ya kuwasili ndege ya Rais Obama kwa sababu za kiusalama.
Kamanda Kato alisema vifaa vitakavyotumika katika ziara hiyo vimeshawasili, yakiwemo magari manne ya mizigo yaliyokuwa na vifaa vya mawasiliano.
Kato alisema magari hayo yaliletwa na ndege tatu zilizotua nchini Jumanne wiki hii na baadaye kuondoka.
Leo saa saba usiku inatarajiwa kuwasili ndege ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari vya Marekani,†alisema.
Alisema wanatarajia pia zitawasili ndege zitakazobeba magari 50, ambayo yatatumika katika msafara wa rais huyo.
Kamanda Kato alisema Rais Obama atawasili na ndege mbili, moja ikiwa ni ya akiba.
Katika hatua nyingine, alisema teksi zinazoegeshwa uwanja wa ndege zitaondolewa Jumatatu na zitarejeshwa baada ya rais huyo kuondoka nchini.
Alisema magari ya wafanyakazi yataruhusiwa kuingia uwanjani baada ya ukaguzi kufanyika.
Kato alisema msafara huo utapishwa kama misafara mingine, na hakuna mawasiliano yatakayokatwa.
Kwa mujibu wa Kato, safari za anga zitakuwa kama kawaida baada ya kiongozi huyo kuwasili.
Aliwaomba wananchi kuwa wavumilivu kutokana na msongamano utakaosababishwa na msafara huo, kwani ziara hiyo ina manufaa kwa taifa.
Uwanjani hapo jana kulikuwa na ulinzi mkali, kukiwa na makundi ya askari wenye silaha waliokuwa wakifanya doria.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema Barabara ya Nyerere haitafungwa kwa saa tano, siku ya ujio wa Rais Obama, kama ilivyoripotiwa kwenye mitandao ya kijamii.
Polisi imesema haijatoa taarifa rasmi ya matumizi ya barabara siku hiyo na kwamba, litafanya hivyo siku moja kabla.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kumekuwa na habari nyingi za upotoshaji kuhusu ujio wa kiongozi huyo, kiasi cha kuwatia hofu wananchi.
Shughuli hazitasimama, mambo yataendelea kama kawaida. Barabara kubwa ya kwanza kutumika itakuwa Nyerere, lakini haitafungwa kwa saa tano kama inavyodaiwa, wananchi wasiwe na hofu,†alisema.
Licha ya ziara ya Rais Obama, Tanzania ina ugeni mwingine mkubwa wa viongozi wakuu wa nchi na marais wastaafu wanaohudhuria mkutano wa Majadiliano ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema barabara zingine zitakazohusika ni zinazoingia katika hoteli kubwa, ambazo zitafungwa kwa muda asubuhi na jioni wakati wa wajumbe wakiingia na kutoka kwenye mkutano.
Katika hatua nyingine, wananchi wamepongeza usafi uliofanyika katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na kutaka suala hilo liwe endelevu.
Pongezi hizo pia zimekuwa zikitolewa kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakisema ˜Dar es Salaam safi inawezekana
Licha ya usafi huo, baadhi ya wafanyabiashara walio kwenye maeneo yasiyo rasmi, wamekaidi kuondoka.
Baadhi ya wafanyabiashara hao waliendelea kupanga viatu, tai na bidhaa nyingine katika maeneo ya Posta, huku walioshika bidhaa mkononi wakiendelea na shughuli zao.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru