na mwandishi wetu
MPANGO wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge nchini (MKURABITA), umeendelea kuwa mkombozi wa watanzania katika kufikia Maisha Bora kwa Kila Mtanzania.
Hatua hiyo imetokana na kuendelea kugawa hati miliki za kimila kwa wananchi mbalimbali nchini ikiwa ni kuwawezesha kupata fursa za mikopo kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Mratibu wa MKURABITA Seraphia Mgembe, alisema hayo juzi wakati akitoa tathimini ya kazi ya kutoa hatimiliki hizo kwa wakulima wa chai katika wilaya za Mbinga, Mufindi na Njombe.
Kazi ya kutoa hatimiliki hizo ni mwendelezo katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo wiki mbili zilizopita wananchi wa wilaya ya Rungwe walikabidhiwa hati miliki za kimila.
Alisema maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kupatikana kwa wananchi kukaa vijiweni ama kubweteka bila kufanya kazi na kusubiri serikali kufanya kila kitu.
Seraphia alisema jukumu la serikali ni kujenga mazingira bora kwa wananchi kuzalisha mali ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri rasilimali walizonazo kama dhamana ya kupata mitaji.
“Tunaendelea kutoa hati miliki za kimila ili kuwezesha wananchi kupata mitaji kwa kutumia rasilimali walizonazo. Kazi inayoafuata ni kuendelea kuwajengea uwezo na jinsi ya kuzitumia kama dhamana,” alisema.
Alisema maendeleo ya kweli na ya haraka ni yale yanayotokana na matumizi ya rasilimali zinazowaunganisha wananchi na MKURABITA imekuwa kiunganishi muhimu baina yao na taasisi za fedha nchini.
Katika hatua nyingine, wakuu wa wilaya za Njombe, Sarah Dumba na Mufindi, Evarista Kalalu, waliipongeza MKURABITA kutokana na jitihada za kuhakikisha wakulima wa chai wanayamiliki rasmi mashamba ili kuwakomboa na umasikini.
Walisema kuwa awali wakulima hao walikuwa na utajiri, ambao haukuwafainisha zaidi ya kulima na kuuza mazao yao, lakini kwa sasa watakuwa wamiliki na pia watatumia hati miliki zao kukopa fedha kwenye taasisi za fedha. Jumla ya hatimiliki za kimila zimetolewa kwa wakulima wa chai.
Tuesday, 25 June 2013
MKURABITA yaonyesha njia ya maisha bora
05:23
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru