Tuesday, 25 June 2013

Pikipiki zageuka chinjachinja


Na Epson Luhwago, Dodoma
AJALI za pikipiki zimeendelea kuwa chanzo cha vifo vya maelfu ya watu nchini, ambapo ndani ya miezi 17 iliyopita zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema bungeni jana kuwa, kuanzia Januari, mwaka jana hadi Mei mwaka huu, watu 1,282 walifariki dunia kutokana na ajali hizo.
Alisema vifo hivyo vilitokana na ajali 8,178 zilizotokea nchi nzima, ambapo Dar es Salaam ndiyo kinara wa matukio hayo kwa kuwa na ajali 3,650.
Kwa mwaka jana, alisema watu 930 walipoteza maisha kutokana na ajali za usafiri huo, na kwa mwaka huu, kuanzia Januari hadi Mei watu 352 walifariki dunia.
“Matukio haya yamesababisha idadi ya vifo na majeruhi kuwa kubwa kiasi cha kuzifanya hospitali nyingi kuanzisha wodi maalumu za majeruhi wa pikipiki,” alisema.
 Dk. Nchimbi alisema matukio hayo ni mengi na ya kutisha, hivyo hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kupunguza tatizo hilo.
Kushindwa kufanya hivyo, alisema kutasababisha vifo viendelee na kuongeza idadi ya walemavu, yatima na watu wasiojiweza, ambao wanakuwa tegemezi.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, ajali hizo zinasababishwa na waendeshaji kutokujua sheria, kanuni na matumizi ya alama za barabarani, mwendo kasi, kupita taa za kuongozea magari bila kuruhusiwa na kuwadharau askari wa usalama barabarani.
Alisema sababu nyingine ni baadhi ya madereva wa magari makubwa kutokuwaheshimu wenzao wa pikipiki, kutokana na kasumba iliyojengeka miongoni mwao kuwa waendesha vyombo hivyo maarufu bodaboda, hawana nidhamu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru