Wednesday, 19 June 2013

Mbowe, Lema wasakwa na polisi

SHAABAN MDOE NA LILIAN JOEL, ARUSHA
JESHI la Polisi limemwamuru Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kujisalimisha kutokana na vurugu zilizotokea juzi jijini Arusha.
Pia limewaonya watu waliowapa hifadhi kuwa wakiendelea kuwaficha na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hilo lilitolewa jana na Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja.
Alisema ni lazima wajisalimishe polisi ili watoa ushahidi kuwa, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) ndio waliolipua bomu kwenye mkutano wa hadhara wa CHADEMA Jumamosi iliyopita, eneo la Soweto, jijini Arusha.
Chagonja anayeongoza timu ya wapepelezi kutoka Makao Makuu ya Polisi, alisema iwapo Mbowe anaona hatatendewa haki, anapaswa kuwasilisha ushahidi huo kwa viongozi wa dini au kwa Rais Jakaya Kikwete, ili kurahisisha kazi ya kuwatia mbaroni wahusika.
Mbowe na Lema wamejificha tangu juzi walipotimua mbio wakati wabunge wenzao wakitiwa mbaroni kwa kosa la kukusanyika bila kibali.
Wabunge waliokamatwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akonaay (Mbulu), Saidi Arfi (Mpanda Mjini) na Joyce Mukya (Viti Maalumu), ambao jana walishindwa kupandishwa kizimbani kutokana na kutokamilika kwa jalada la kesi.
Watuhumiwa hao na wafuasi 67 wa CHADEMA walitiwa mbaroni juzi na jana waliachiwa kwa dhamana, ambapo huenda wakapanda kizimbani leo.
Katika tukio la juzi, polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi na viongozi wa chama hicho waliokusanyika viwanja vya Soweto. Pia baiskeli 16, pikipiki 106 na magari sita, likiwemo linalotumiwa na Mbowe yanashikiliwa polisi.
Kamishna Chagonja alisema ni vyema wakatii sheria kwa kujisalimisha mikononi mwa polisi, badala ya kusubiri jeshi litumie nguvu kuwakamata.
Alisema hali ya amani imerejea jijini Arusha, ambapo wananchi wanaendelea na shughuli za uzalishajimali.
Kamishna Chagonja aliwataka wananchi kupuuza vitisho vinavyotolewa na wafuasi wa chama hicho, kwani polisi wapo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao.

WABUNGE KUADHIBIWA
Katika hatua nyingine, wabunge wa CHADEMA wameendelea kutohudhuria vikao vya Bunge bila taarifa au kupewa ruhusa.
Wabunge hao wakiongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mbowe, hadi jana hawajahudhuria vikao vitatu, huku wenzao wakiendelea kujadili hotuba ya bajeti ya serikali.
Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema hana taarifa za kutokuwepo kwa wabunge hao bungeni.
Mkurugenzi wa Idara za Shughuli za Bunge, John Joel, alisema jana kuwa, hakuna taarifa kuhusu kutokuwepo kwa wabunge hao na kwamba, kwa mujibu wa kanuni ni kosa.
Alisema kutokuwepo kwao kunahesabiwa kuwa utoro na kwamba, licha ya kuwa ni kinyume cha kanuni, lakini kunaathiri mwenendo wa Bunge.
“Kikanuni mbunge akitaka kuondoka ni lazima atoe taarifa kwa spika, ambaye ataangalia iwapo hakutakuwa na athari kwa shughuli za Bunge. Bunge halina taarifa kuhusu kutokuwepo kwao,” alisema.
Hata hivyo, alisema Bunge linaendelea kuweka sawa kanuni ili kuwabana zaidi wabunge na kwamba, watoro wote hawatalipwa posho za vikao.
“Wabunge ambao hawako bungeni bila ruhusa hawatalipwa posho, kwa sababu tunatoa kwa wanaohudhuria vikao,” alisema.

WALIPULIWA KWA UCHOCHEZI
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangallah, ameitaka CHADEMA kuacha kufanya siasa za vurugu.
Akichangia hotuba ya bajeti ya serikali bungeni jana, alisema kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, wakiwemo CHADEMA, zinaathiri amani na utulivu.
Dk. Kigwangallah alisema siasa ni uchumi na kwamba, kuendelea kuhamasisha vurugu kamwe hakuwezi kuliondoa taifa kwenye umasikini.
“Kauli aliyotoa Mbowe kuwa ana ushahidi kuhusu aliyehusika na tukio la kurusha bomu katika mkutano wake ni tata na inaacha maswali mengi,” alisema.
Alisema ni vyema Mbowe kama ana ushahidi akaupeleka polisi ili ufanyiwe kazi na wahusika wakamatwe, lakini hatua yake ya kukimbia inatia shaka.
“Anapodai ana ushaidi wa video kuhusu tukio hilo, nani alipiga na yeye alikuwa wapi hadi aone uhalifu ukitendeka na akae kimya. Aseme ametumia chombo gani kuwabaini wahusika,” alisema.

WASOMI WAPONDA
Katika hatua nyingine, wasomi nchini wamewashukia wanasiasa na kuwataka kuacha siasa za kiharakati, kwa kuwa mara nyingi zinasababisha vurugu.
Pia wametakiwa kujifunza kuendesha vyama kwa ustaarabu, kuhamasishana kutii sheria na kuviacha vyombo vya usalama kutekeleza wajibu wake bila ya kuingiliwa.
Hata hivyo, serikali kupitia vyombo vya dola imetakiwa ichuke hatua madhubuti ili kudhibiti uvunjifu wa amani.
Mhadhiri wa Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohammed Bakari, alisema nchi iliamua kufuata siasa ya vyama vingi, hivyo ina wajibu wa kufuata sheria kwa sababu vyama vililetwa na sheria.
"Baadhi ya watu wanaendesha siasa za harakati, ambazo zinaleta vurugu. Kama tumeamua kufuata vyama vingi tuna wajibu wa kufuata sheria kwa sababu vyama vingi viliruhusiwa kwa mujibu wa sheria," alisema.
Bakari alisema demokrasia inatakiwa iambatane na wajibu wa kufuata sheria, hivyo kisitokee kikundi cha watu au mtu yeyote akasababisha uvunjifu wa amani kwa madai ya demokrasia, kwani demokrasia bila sheria ni vurugu.
Naye Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema matukio yaliyotokea Arusha yanapaswa kuangaliwa kwa upana zaidi.
Alisema jamii inatakiwa kujiuliza kwa nini matukio kama hayo yanajirudia mkoani humo.
Dk. Bana alisema vyama vya siasa vinatakiwa vijifunze kuendesha shughuli kwa njia za kistaarabu na kutii sheria.
Alisema hakuna chama chenye uwezo wa kuchunguza matukio ya kihalifu, ukiwemo wa jinai, hivyo alishauri suala hilo liachwe kwa vyombo husika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Dk. Augustine Mrema, aliwataka wanasiasa kuwa makini kwa kauli na matendo yao, kwani yanaweza kulisambaratisha taifa.
Alisema wanasiasa nchini wanatakiwa kuwa makini na baadhi ya vitendo vyao, ambavyo havina tija kwa maendeleo ya taifa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru