Tuesday, 25 June 2013

Gharama huduma za simu



Na waandishi wetu, Dar na Dodoma

SERIKALI imesema itaanza kuzibana kampuni za simu ili zilipe kodi na mapato stahili, pia kuwashirikisha Watanzania katika umiliki wake.

Katika kufanya hivyo, imesema itaweka mtambo maalumu wa kufuatilia miamala yote ya kampuni hizo na kuziingiza katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).
    
Serikali imesema kamwe gharama za huduma za simu hazitaongezwa, kwa kuwa kuziongeza ni kuwanyonya Watanzania, kwani gharama za uendeshaji zimeshuka kwa kiwango kikubwa.

Naibu Waziri wa Fedha, Janet Mbene, akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/2014, alisema suala la kampuni za simu kutokulipa kodi stahili limekuwa kilio cha muda mrefu.

Alisema ili kuhakikisha serikali inapata mapato hayo, kampuni hizo kuanzia mwaka ujao wa fedha zitawekewa mtambo maalumu utakaofuatilia miamala na viwango vyote vinavyotozwa na kampuni hizo. 

Kwa mujibu wa Janet, mtambo huo maalumu utakuwa ukisimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Mtambo huu utasaidia kudhibiti wizi wa aina yoyote na kubaini miamala ya fedha ndani ya kampuni hizo, pia kutambua kama kuna udanganyifu wowote unaofanywa,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema serikali imeanzisha vikosi kazi kwa ajili ya kuzifuatilia kampuni hizo ili kuhakikisha zinaingizwa kwenye orodha ya kampuni zilizoko DSE.

Saada alisema vikosi kazi hivyo vinatokana na sheria mpya inayolenga kuzidhibiti kampuni hizo na vitakuwa chini ya TCRA na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya kudhibiti kampuni za madini nazo kuingia katika soko la hisa. 

Alisema Kampuni ya Airtel imeorodheshwa kwenye soko hilo pamoja na zingine za sukari za Kilombero na Mtibwa, Saruji Mbeya, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Kampuni ya Mabati ya ALAF Limited na kampuni ya vyombo vya umeme ya TANELEC.

Kampuni hizo zinaungana na Benki ya NMB, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), TOL Gases Limited, Swissport, Saruji Tanga na CRDB.

“Kuingia kwa kampuni hizo katika soko la hisa, kutawawezesha Watanzania kupata fursa katika umiliki na kuendesha uchumi wa nchi.

Wabunge waliochangia bajeti walisema serikali imekuwa ikikosa mabilioni ya shilingi kwa mwaka kutokana na kampuni za simu kutokulipa fedha kupitia huduma mbalimbali zinazotoa kwa wateja.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema kampuni hizo zinatumia gharama ndogo kujiendesha hivyo, gharama kwa watumiaji zinapaswa kupungua zaidi na si kuongezeka.

Alisema kwa sasa serikali ipo katika mchakato wa kuangalia gharama za uwekezaji katika kampuni hizo ili iweze kukusanya kodi inayostahili, kwa kuwa kuna udanganyifu mkubwa.

“Tusingependa wananchi waathirike wala kubebeshwa mzigo wa gharama, kampuni hizi zinatumia gharama ndogo kujiendesha kwa kutumia mkongo wa taifa wa mawasiliano,” alisema.

Alisema kampuni hizo zimevunja  sheria ya soko huria kwa kukutana na kupanga kupandisha gharama kinyume cha sheria.

“Hairuhusiwi kisheria kampuni zinazofanya biashara moja kukaa na kukubaliana kupandisha gharama, huo si ushindani na suala hili halikubaliki,” alisema.

Kampuni hizo kupitia Chama cha Wamiliki wa Simu za Mkononi Tanzania (MOAT), zimetangaza gharama za matumizi ya simu zitapanda kuanzia Julai Mosi, mwaka huu. 

Hatua hiyo imeelezwa huenda  inatokana na serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 kueleza itazitoza kodi kwa asilimia 14. 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru