Wednesday, 19 June 2013

KUTOKA BUNGENI DODOMA

Mgogoro wa ardhi Mpendae kutatuliwa

MGOGORO wa ardhi kati ya wananchi wa Mpendae na kambi ya jeshi ya Bavuai, Zanzibar,   unatarajiwa kupatiwa ufumbuzi baada ya serikali kuamua kupima maeneo hayo katika mwaka ujao wa fedha.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema jana kuwa, mgogoro huo utamalizwa baada ya kupimwa kwa maeneo ya kambi hiyo ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Nahodha alisema katika upimaji, iwapo itabainika jeshi limechukua eneo la wananchi, wahusika watalipwa fidia na kwa upande mwingine ikijulikana wananchi ndio waliovamia, watalazimika kuondoka.
“Kimsingi serikali haina sababu ya kuwa na mgogoro na wananchi, ndiyo maana imeamua kupima maeneo ya kambi hii ili kuweka wazi mipaka na hatimaye kumaliza tatizo hili,” alisema.
Katika hatua nyingine, Nahodha alisema nchini kuna zaidi ya migogoro 80 inayohusisha wananchi na kambi za jeshi.
Akijibu swali la nyongeza la Ester Bulaya, aliyetaka kujua kuna mpango gani wa kutatua migogoro hiyo, ukiwemo wa kambi ya Kunduchi, Dar es Salaam, waziri alisema serikali imeanza kuipatia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Nahodha, mgogoro wa ardhi wa Kunduchi uko katika hatua nzuri ya kupatiwa ufumbuzi na kwamba, baada ya mkutano wa bunge, atatembelea eneo hilo pamoja na mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), kuona namna ya kufikia suluhu.

 

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru