Tuesday 29 October 2013

CHADEMA yapasuka


Na waandishi wetu
HALI imezidi kuwa tete ndani ya CHADEMA kufuatia aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuanza kufichua madudu yaliyoota mizizi na udhaifu wa viongozi.
Mwigamba, ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alishushiwa kipigo na viongozi wenzake kisha kusimamishwa uanachama kwa tuhuma za usaliti, amesema baadhi ya wajumbe wa kamati kuu na wenyeviti wa mikoa 12 wametangaza kumuunga mkono.


Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mwigamba amesema viongozi wenzake hao wamesema watamuunga mkono, na kwamba wamekuwa wakikerwa na uozo na madudu yanayofanyika ndani hya CHADEMA.
Bila kuwataja viongozi walimpigia simu na kumpongeza kwa uamuzi wa kuweka mambo hadharani na kutangaza kumuunga mkono, Mwigamba amesema wanachama na baadhi ya viongozi hawaridhishwi na mambo yanavyokwenda, lakini wanashindwa kusema kwa kuogopa kushughulikiwa.
Amesema wajumbe watano wa kamati kuu, wenyeviti wa mikoa 12 Bara na Zanzibar pamoja na wenyeviti wa wilaya zaidi ya 20 na makatibu wao, wamemweleza amechukua uamuzi sahihi wa kuwapsha viongozi kuhusu udhaifu, ikiwa ni pamoja kukifanya chama hicho kama taasisi binafsi.
“Ndio nimeanza kazi ya kukisafisha chama kwa maslahi ya wanachama wote na Watanzania, mambo yanayovyokwenda si sawa na tukiendelea hivi tukipewa nchi tutaiharibu na kuwafanya watu wajute.
“Viongozi wenzangu wametangaza kuniunga mkono na wako nyuma yangu licha ya wachache kuniita msaliti kwa kusema ukweli,’’ alisema Mwigamba.
Pia, alisema bado ana siri nyingi kuhusu madudu yanayoendelea ndani ya CHADEMA, na kwamba viongozi wakiendelea kumdhalilisha kwa kumwita msaliti licha ya kumshushia kipigo, ataweka hadharani yote.
“Kwa muda mrefu nimekuwa mwanachama na kiongozi mzalendo kwa chama changu, lakini viongozi wachache mamluki wameamua kunidhalilisha na kuniangamiza, kabla ya kunifukuza makao makuu nilikuwa mhasibu, hivyo uchafu wote naujua,’’ alionya Mwigamba.
Hata hivyo, Mwigamba amesema kuwa baadhi ya wanachama wachache ambao anaamini hawafahamu uchafu unaofanyika ndani ya CHADEMA, wamempigia simu na kumtuhumu kutaka kukisambaratisha chama.
Amesema viongozi na wanachama wa mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Shinyanga, Mara, Tabora na hata sehemu kubwa ya Zanzibar, wamempigia na kumweleza wako pamoja, lakini wachache wamemlaumu kwa uamuzi wake huo.
“Wengi wanaumia na mambo yanavyokwenda katika hiki chama, kwa nje kinaonekana kisafi, lakini ndani kimeoza. Kuna ukiukwaji mkubwa wa Katiba, hakuna uchaguzi na mbunge wa jimbo anatoka Arusha ila viti maalumu anapewa wa Kilimanjjaro,’’ alisema na kuongeza:

“Hawa si kosa lao, kwani hawaingii ndani ya vikao, wanachofahamu ni kutakiwa kukunja ngumi na kupiga kelele tu, vinginevyo wangenielewa hiki ninachokisema”.
Afichua madudu ya Lema Arusha
Mwigamba ameweka bayana kuwa kuna hatari kubwa ya CHADEMA kupoteza jimbo la Arusha kutokana na ahadi zilizotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Godbless Lema, kutotekelezwa huku kukiwa na visingizio mbalimbali.
Amesema Lema anadaiwa ahadi nyingi, ikiwemo ujenzi wa Machinga Complex alioliahidi kwa wafanyabiashara, hospitali ya kinamama na watoto, kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoani kutoka Mjini kwenda Kisongo na mengine mengi.
Hata hivyo, amesema ahadi hizo haziwezi kutekelezwa kutokana na Lema kubeba ajenda za ubabe na fitina na kuacha maendeleo kwa wapigakura wake.

Asisitiza kumvaa Mbowe
Mwigamba, ambaye juzi alilalamika kuwa alishambuliwa na viongozi wenzake, huku Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, akishuhudia, amesema kamwe hatasita kumweleza udhaifu wake katika uongozi.
Amesema Mbowe alishuhudia mwanzo hadi mwisho wakati akishushiwa kipigo kabla ya kukabidhiwa kwa polisi, na kwamba kamwe hilo haliwezi kumfunga mdogo kueleza mfumo mbovu wa uongozi ndani ya chama hicho.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru