Tuesday 29 October 2013

Membe aongoza mamia kumuaga Balozi Sepetu


NA RACHEL KYALA
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa marehemu Balozi Isaac Sepetu unaotarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Mbuzini, Zanzibar.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo nyumbani kwa marehemu Sinza, Dar es Salaam, Waziri Membe alisema Taifa limepoteza kiongozi mzuri na mwenye uzoefu mkubwa katika kazi aliyewaheshimu, kuwapenda na kuwathamini watu wote.
“Marehemu ameacha majonzi kwa watu wake, kwani alikuwa kiongozi mchapakazi na mwadilifu, alikuwa mfano wa kuigwa, amefanya mengi mazuri kwa nchi yake na ameondoka bila dosari yoyote katika utumishi wake,” alisema.
Aidha, Waziri Membe aliongeza kuwa, marehemu alikuwa mtu aliyekataa mabaya kwa nguvu zake zote, hususan suala la rushwa na atakumbukwa daima na watu wote.
“Natoa pole kwa familia na ninawaombea ndugu, jamaa na marafiki wote Mwenyezi Mungu awape nguvu haraka ili kuweza kuendelea na ujenzi wa taifa,” alisema.
Viongiozi wengine walioeleza jinsi walivyomfahamu marehemu ni Mama Getrude Mongela, ambaye alisema kuwa katika maisha yake ya siasa alikuwa mtu mwadilifu na aliyechukia majungu.
Marehemu Balozi Sepetu alizaliwa Oktoba 16, 1943 wilayani Sikonge, Tabora na baadaye alichukuliwa na baba yake mkubwa mareheu Said Sepetu Kilanga na kuhamia visiwani Zanzibar alikokulia na kusoma shule.
Mwaka 1952 hadi 1963, marehemu alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya St. Joseph’s (Tumekuja), Zanzibar ambapo mwaka 1964 hadi 1970 alipata Shahada ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Berlin, Ujerumani.
Mwaka 1971 hadi 1972 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Zanzibar.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru