Wednesday 30 October 2013

Mbunge CHADEMA ataka wananchi waiamini CCM


NA Stephen baligeya, DODOMA
MBUNGE wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John Shibuda, amemwagia sifa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, kwa kumwelezea kuwa kiongozi mtendaji makini, mchapakazi na msikivu katika kushughulikia kero za wananchi.
Pia, alisema CCM ni chama sikivu katika kusikiliza kero za wananchi, hivyo kutakiwa kuwa na imani nacho ili matatizo mbalimbali yaweze kutatuliwa.
Kauli hiyo ya Shibuda, ambaye ni mwanasiasa makini na muwazi, alisema linapokuja suala la maendeleo na uzalendo kwa taifa, inadhihirisha namna CCM na serikali yake wanavyotimiza wajibu katika kuwatumikia Watanzania bila kujali itikadi.
Hayo aliyaeleza wakati wa mkutano wa pamoja kati ya wawakilishi wa wafugaji kutoka wilaya mbalimbali za mikoa ya Dodoma, Mbeya na Morogoro ulioandaliwa na Kinana katika kusikiliza kero zinazowakabili.
Alisema Kinana amekuwa kiongozi mchapakazi na makini katika kazi zake, hivyo kuwataka wafugaji hao kuwa na imani naye katika kushughulikia kero mbalimbali walizozieleza kwake, kwa kuwa ataziwasilisha katika sehemu husika.
ìMwamini huyu na kwa kuwa hata chama anachokiongoza ni sikivu kwa wananchi wake, matatizo yenu ya kukosa sehemu za malisho, migogoro kati yenu na wakulima itatatuliwa kwa haraka,î alieleza Shibuda.
Vilevile, aliwahakikishia kuwa, kwa kuwa katika mkutano huo alikuwepo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye amekulia katika nyumba isiyojua dhuluma, basi matatizo yao yatashughulikiwa kwa haraka.
Katika kikao hicho, wafugaji hao walikuwa wakilalamikia ‘Operesheni Tokomeza’ ambayo inalenga kupambana na majangili wa meno ya tembo, ambapo katika operesheni hiyo wafugaji walieleza kunyanyaswa kwa kuchukuliwa mifugo yao, kulipishwa faini kwa kuitwa wahamiaji haramu.
Katika kulishughulikia tatizo hilo, Kinana alieleza kutokana na malalamiko hayo amegundua kuwa, tatizo kubwa lililopo ni kati ya wakulima na wafugaji, wafugaji na hifadhi za taifa na mchakato wa Operesheni Tokomeza.
ìMgogoro kati yenu na wafugaji ni kutokana na nyinyi kudaiwa kuingiza mifugo yenu katika mashamba, lakini pia wakulima kulima sehemu ya malisho ya mifugo. Vilevile, kumekuwa hakuna uhusiano wa karibu kati ya wafugaji na hifadhi, hivyo kuongeza migogoro,î alieleza.
Kinana alisema kuwa Operesheni Tokomeza ina nia njema ya kupambana na majangili wa meno ya tembo, lakini imepata changamoto kadhaa, ikiwemo baadhi ya wanaoiendesha kuvuka mipaka kwa kuonea watu.
Alisema kuhusu malalamiko ya suala hilo, tayari yameshamfikia Rais Jakaya Kikwete na ameshaagiza mawaziri wanaohusika kulishughulikia ili kuondoa kasoro ambazo zimeanza kujitokeza.
ìMimi nimesikia malalamiko na vilio vyenu, nitawasilisha serikalini na kuonana na Waziri Mkuu na nitawaita tena ili mje kusikia ni hatua gani zimechukuliwa katika kushuguklikia matatizo ya wafugaji.
ìBinafsi najua mkipata sehemu ya malisho, majosho na mabwawa hamtakuwa mnahamahama na kuitwa wahamiaji haramu, hivyo ni wajibu wa serikali kuhakikisha miundombinu ya maji, majosho na kutenga sehemu ya malisho,î alieleza.
Alisema Kamati Kuu ya CCM iliyopita iliona tatizo la wafugaji na wakulima na kuitaka serikali kulifanyia kazi na kwa kuwa yeye ni mtendaji wa Chama, atahakikisha anasimamia serikali kwa kuwa ndio wajibu wake kutekeleza Ilani ya Chama.
Dk. Nchimbi alieleza kuwa tayari mawaziri watatu wameshakutana ili kuona kasoro zilizoanza kujitokeza katika operesheni hiyo ili kuziondoa na kutoleta usumbufu kwa wananchi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru