Wednesday 30 October 2013

Mtumishi KADCO apigwa risasi akidhaniwa jambazi


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
POLISI waliokuwa lindo katika benki ya CRDB tawi lililopo katika jengo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jijini hapa, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi begani mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Violeth Mathias (33).
Inadaiwa kuwa walihisi mwanamke huyo mkazi wa Njiro, alitaka kutekeleza tukio la ujambazi katika benki hiyo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema lilitokea jana saa 6.45 mchana, wakati mwanamke huyo ambaye ni mtumishi wa shirika la uwakala wa uendeshaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO), alipofika katika eneo hilo akiwa na gari aina ya Toyoto Mark, lenye namba za usajili T888 BWW.
Kamanda Sabas, alisema Violeth alifika na gari hilo na kupaki mbele ya mlango mkuu wa kuingilia katika benki hiyo jambo lililowasababisha askari hao kumuamuru kulisogeza gari lake mbele ili kupisha njia, lakini aligoma.
Alisema baada ya kugoma, askari hao walimlazimisha kwa nguvu na ndipo  kulizuka zogo kubwa na kisha askari hao waliamua kutoa upepo katika magurudumu ya gari hilo ili kumdhibiti.
Kamanda huyo, alisema kufuatia kitendo hicho cha gari lake kutolewa upepo, Violeth alishuka kwenye gari na kuchomoa bastola yake katika pochi, huku akimuelekezea mmoja wa askari hao kwa lengo la kumdhuru.
Ndipo askari mwingine aliamua kujikinga kwa kumfyatulia risasi mwanamke iliyompata katika bega la mkono wa kushoto.
Kamanda Sabas, alisema baada ya risasi hiyo kumpata, alianguka chini na walimkamata na kumpeleka katika Kituo cha Polisi Kati, jirani kabisa na benki hiyo kwaajili ya kuandikisha maelezo na kisha alipelekwa Hospitali ya Mount Meru akiwa chini ya ulinzi kwaajili ya matibabu.
Kamanda Sabas, alisema kwa mujibu wa sheria, hairuhusiwi gari lolote kusimama mbele ya lango kuu la kuingilia benki, kitendo kilichofanywa na mwanamke huyo.
 “Na hata pale alipoelekezwa cha kufanya alikaidi,” alisema Kamanda huyo.
Hata hivyo, Kamanda Sabas alisema kufuatia tukio hilo, Polisi wanaendelea kumshikilia  mwanamke huyo pamoja na mwenzake aliyekua naye kwenye gari kwaajili ya upelelezi zaidi.
“Askari wamekueleza ondoa gari, hapo hairuhusiwi kuegesha halafu wewe unakaidi na kisha unataka kuwapiga askari kwa risasi kama kweli huna nia mbaya.
“Tunamshikilia yeye na mwenzake mmoja kwa upelelezi zaidi ili tujiridhishe na tujue dhamira yao ilikuwa nini,” alisema Kamanda Sabas.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru