Tuesday 15 October 2013

JK asaidia yatima na wazee vyakula


NA MAGRETH  KINABO WA MAELEZO
RAIS Jakaya Kikwete, ametoa msaada wa vyakula kwa makundi mbalimbali, yakihusisha wazee na wasiojiweza, watoto yatima na watoto walio katika mkinzano na kisheria kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Edi El Hajj.
Msaada huo ulitolewa jana kwa niaba ya Rais  Kikwete, na Kaimu Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Rabirira Mushi katika hafla fupi iliyofanyika kwenye mahabusu ya watoto Regency, Dar es Salaam kwa vituo na makazi 12 ya makundi hayo yaliyopo nchini unaogharimu sh. milioni 5.5.
ìRais ametoa zawadi ya mbuzi, mchele na mafuta ya kupikia ili kuona kwamba watoto na wazee hawa wanajumuika na wanajamii wengine katika sherehe hii,î alisema Rabirira.
Alivitaja vituo vilipata msaada huo na maeneo vilivyoko kwenye mabano kuwa Kituo cha Watoto Dar  Al Arkam na Nunge (Temeke) na Msongola Orphaned Centre (Ilala).
Vingine ni Furaha (Kinondoni), Mother Theresa (Mburahati), Malaika Kids Home (Mkuranga) na Makazi ya Wazee na Wasiojiweza cha Kilima (Bukoba Vijijini).
Vituo vingine ni Mahabusi ya Watoto (Arusha Mjini), Mahabusi ya Watoto (Tanga Mjini), Makazi ya Wazee Mwanzange (Tanga), Makao ya Watoto Istikama (Pemba) na Makazi ya Wazee Sebuleni(Unguja).
Akizungumzia kuhusu msaada huo kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Kituo cha Msongola Orphaned Trust Fund, Shanta Deus, alimshukuru Rais Kikwete kwa moyo wake wa kujitolea kwa makundi hayo, huku akiwataka watu wengine kuiga mfano.
ìNinawaomba watu wengine, sekta binafsi na kampuni mbalimbali kuiga mfano huu ili kuwasaidia watoto yatima na wanaoshi katika mazingira hatarishi pamoja na makundi maalumu kwa kutoa misaada mbalimbali,” alisisitiza Shanta.
Naye Sista Oliver Paulo ambaye ni mlezi wa makao ya watoto yatima, Kijiji cha Furaha aliishauri jamii iwe na tabia ya kushirikiana na makundi hayo katika sherehe mbalimbali na kuwasaidia.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru