Tuesday 22 October 2013

Kodi ya ving’amuzi kuangaliwa-January


NA LILIAN JOEL, ARUSHA
WIZARA ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inakusudia kuwasilisha mapendekezo serikalini ya kupunguza au kuondoa kodi kwenye ving’amuzi ili kuwapunguzia gharama wananchi.
Hayo yalisemwa jijini Arusha jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, January Makamba, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa 21 wa Umoja wa Taasisi za Utangazaji za Nchi za Kusini mwa Afrika (SABA), unaoendelea jijini hapa.
Alisema sababu ya kupunguza ama kuondoa kabisa kodi hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania wengi kumudu kununua vifaa hivyo na kupata huduma ya utangazaji wa runinga bila usumbufu.
Naibu Waziri huyo, alisema ili kufanikisha lengo hilo, wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, inawasiliana na Wizara ya Fedha na wadau wengine, kuangalia njia muafaka wa kufikia malengo hayo yatakayoleta nafuu kubwa kwa wananchi.
Alisema kwa sasa, wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kununua ving’amuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa malengo ya kimataifa ya kuhamia katika mfumo wa dijitali kutoka analojia.
“Ni faraja kubwa kwamba nchi zingine zinakuja kujifunza kwetu jinsi tulivyofanikiwa kutekeleza mipango ya kuhamia dijitali kutoka analojia. Ingawa tuna safari ndefu, lakini tunajivunia maendeleo tuliyoyafikia,” alisema Profesa Mkoma.
Serikali inatekeleza mpango wa kuzima mitambo yote ya analojia kuanzia mapema mwaka huu, huku ikikusudia kuwa ifikapo mwaka 2015, matangazo yote ya televisheni na radio yatarushwa kwa dijitali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru