Thursday 17 October 2013

DPP amngíangíania Zombe


NA FURAHA OMARY
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imempa siku 14 kuanzia jana, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kuwasilisha hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufani dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe, na  wenzake wanane.
Hatua hiyo, inatokana na Jaji Aloyisius Mujuluzi wa Mahakama hiyo, kukubali ombi la DPP la kuruhusiwa kuwasilisha taarifa hiyo, nje ya muda.
DPP aliwasilisha maombi hayo, baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania, kutupilia mbali rufani yake dhidi ya Zombe na wenzake kutokana na kubaini kuwepo kwa kasoro katika hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufani.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Mujuluzi alisema anakubaliana na ombi la DPP la kuwasilisha dukuduku lake Mahakama ya Rufani dhidi ya hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Salum Massati. 
Jaji Mujuluzi alisema rufani ni haki ya kila mdau mbele ya mahakama ikiwemo umma ambao unawakilishwa kupitia ofisi ya DPP.
Alisema hoja iliyopo si kwamba mahakama ilikuwa sahihi au ilikosea katika kufikia uamuzi wake, bali suala lililopo mahakama ilitafsiri msimamo wa kisheria na kufikia uamuzi uliofikiwa.
"Kwa maslahi ya umma wangetaka kuona mahakama ya juu inachambua vipengele vya kisheria vilivyofikia uamuzi ili kuwa na mwelekeo sahihi kwa uamuzi mwingine," alisema.
Pia, alisema katika maslahi yao ya umma si ya kuachiwa au kutoachiwa kwa waleta maombi, bali walitaka kuona haki inatendeka na kuonekana imetendeka machoni mwa watu.
"Mahakama inaruhusu maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufani dhidi ya uamuzi uliotolewa na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu, Massati," alisema na kuongeza kuwa DPP anaongezewa siku 14 kuanzia jana kuwasilisha taarifa hiyo.
Mbali na Zombe, wajibu maombi mengine ni  ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Awali, DPP alikata rufani Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Zombe na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro na dereva teski mmoja wa Manzese, Dar es Salaam. 
Mei 8, mwaka huu, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufani hiyo kutokana na kubaini kasoro za kisheria ambapo katika hati ya taarifa ya kusudio la kukata rufani waliandika wanapinga hukumu iliyotolewa na Jaji Massati wa Mahakama ya Rufani badala wa jaji wa Mahakama Kuu.
Katika uamuzi wake wa kutupilia mbali rufani hiyo, jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani chini ya Jaji Edward Rutakangwa akishirikiana na Bethuel Mmila na Jaji Salum Mbarouk, lilitoa fursa kwa DPP kukata rufani nje ya muda kwa kuzingatia Sheria ya Ukomo wa Muda, kwa kuwasilisha kwanza maombi ya kuruhusiwa kukata rufaa nje ya muda.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru