Sunday 27 October 2013

Tamati ya CHADEMA imewadia


Na waandishi wetu
BAADA ya viongozi wa CHADEMA kumshushia kipigo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, hali imezidi kuwa tete na viongozi waandamizi ndani ya chama hicho wamesema muda wa kusambaratika umewadia.
Pia, wamesema ubabe wa baadhi ya viongozi na kunajisiwa kwa demokrasia kamwe hakuwezi kuwa mwarobaini wa kukinusuru chama hicho zaidi ya kuongeza kasi ya kukitafuna kwa kasi.
Mwigamba, ambaye anatajwa kuwa mhimili mkubwa na muhimu katika chama hicho mkoani Arusha, alishambuliwa na viongozi wenzake pamoja na walinzi wa Red Brigade kwa madai ya kuwa msaliti, huku kiongozi mmoja akidaiwa kumtolea bastola.
Kiongozi huyo alishambuliwa na wenzake wakati wa kikao cha Baraza la Uongozi wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, kwa kile kilichoelezwa na baadhi ya viongozi waandamizi kuwa hatua ya kuwapasha viongozi wa juu kuhusu mgawanyo wa ruzuku na ukomo wao wa kukaa madarakani.
Katika taarifa yake, Mwigamba alilipua bomu akiwatuhumu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilboard Slaa, kuwa wamechakachua katiba ili waendelee kukaa madarakani.
Hata hivyo, Mwigamba ambaye kwa sasa amesimamishwa uanachama na kuvuliwa uongozi, amesema ataeleza chanzo cha tukio zima na jinsi alivyotaka kuuawa ndani ya ukumbi wa mkutano.
Pia, amesema amewasiliana na mwanasheria wake kwa ajili ya kufungua kesi, na kwamba chanzo cha yeye kupigwa na kudhalilishwa ni kiongozi mmoja ambaye ni mamluki na mwenye maslahi binafsi ndani ya chama hicho.
Akizungumza na UHURU jijini hapa jana, Mwigamba amesema kwa muda mrefu amekuwa muwazi na mzalendo kwa CHADEMA na kwamba, amekuwa masikini na fukara kwa ajili ya kutumia rasilimali zake kwa ajili ya chama hicho.
‘’Siku zote nimekuwa muwazi na mzalendo kwa ajili ya chama, lakini leo nimedhalilishwa na kupigwa kwa ajili ya mtu mmoja mamluki ambaye ana maslahi binafsi ndani ya chama. Lakini mwisho wake umefika, leo nitaeleza kila kitu tangu mwanzo,’’ alisema Mwigamba.
Wakizungumza na UHURU kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi waandamizi wa CHADEMA (majina yanahifadhiwa), walisema suala la matumizi mabaya ya fedha za ruzuku litakizamisha chama hicho.
Wamesema viongozi walipaswa kuwaeleza wanachama ukweli, lakini kila wanapoulizwa au kuhojiwa katika vikao huwa wakali na kuwaziba midomo kwa ubabe kama walivyofanya kwa Mwigamba.
Walisema kilichozungumzwa na Mwigamba ni jambo la msingi na ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu tangu enzi za marehamu Chacha Wangwe (mbunge wa Tarime). Wangwe alifariki dunia kwa ajali yenye utata eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma, ambapo aliwahi kuingia kwenye mzozo mzito na uongozi wa juu wa CHADEMA kuhusu suala la matumizi ya ruzuku.
‘’Kilio cha Mwigamba hakina tofauti na cha marehemu Wangwe na viongozi wengine wa chini, lakini wachache ndio wana uwezo wa kusimama na kuhoji, japo hushambuliwa. Lakini mambo si mazuri na CHADEMA imefikia njiapanda ya kusambaratika,’’ alisema kiongozi mmoja.
Licha ya kuwepo kwa mpasuko wa muda mrefu ndani ya CHADEMA kutokana na kuwepo kwa upendeleo, hali imekuwa mbaya zaidi pale Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, kutaka vyama ambavyo hesabu zake hazikaguliwa kufutiwa ruzuku.
Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alisema vyama vichache ndio hesabu zake zimekaguliwa, huku vingine ikiwemo CHADEMA vikiwa havijawasilisha taarifa za ukaguzi wa hesabu kwa muda mrefu.
Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na baadhi ya viongozi waandamizi ndani ya CHADEMA wakidai itasaidia kurejesha nidhamu ya fedha za ruzuku.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Anthon Komu, aliibuka na kudai hesabu za chama hicho zimekaguliwa na kuishambulia kamati ya Zitto kuwa imedanganya umma.

HUU NDIO WARAKA UNAODAIWA KUSAMBAZWA NA
MWIGAMBA NA KUZUSHA TAFRANI KUBWA CHADEMA
KUFUATIA malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na udhaifu mwingine ambao tumeushuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwa wana-CHADEMA wote nchini kwamba, wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wa chama.
Kihistoria, CHADEMA kati ya mwaka 2005 na 2010, ajenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili. Kupiga vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dk. Slaa na ile ya utetezi wa rasilimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa matukio.

Naandika nikiwa mwana-CHADEMA safi na nataka kila mwanachama atakayesoma atulie na kutafakari. Hili siyo jambo la ushabiki. Ni mawasiliano baina yetu wana-CHADEMA na tunahitaji tutulie na kutafakari.
Nimekuwa mwanachama wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya chama kwa nyakati tofauti, kwa hiyo naelewa ninachokiandika. Nadiriki kusema kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu kwamba CCM inaendelea kutupatia matukio, lakini CCM na serikali yake wakitunyima matukio, CHADEMA chini ya Mbowe, Katibu Mkuu Slaa na Naibu Zitto utakuwa ndo mwisho wake.
CHADEMA iliyopiga kelele sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele hadi sheria ya vyama vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM kumshambulia Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha zilizokaguliwa.
Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake nini? Kama chama kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake hofu ni ya nini? Si wasubiri kikao na kamati ya bunge. Katibu mkuu aende na hizo ripoti na nyaraka zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?
Napenda kabla sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza, ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wa kutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia mwingine kidemokrasia bila vurugu.
Hawakuwa madikteta na nawapongeza sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi imara inayojali demokrasia na haki ya kila mwanachama.
Ni kwa msingi huo, waliamua kuandika kabisa katika katiba yetu kwamba kiongozi yeyote katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea na kuongoza kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada yapo hawezi kugombea tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba walimaanisha kile walichokisema, wote wawili hawakuwahi kukaa madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika katiba, bali wote wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Napenda pia kumpongeza mwenyekiti aliyepo madarakani, Mbowe. Kuna mengi amekifanyia chama. Kakitoa kutoka kwenye chama cha tatu ama nne kwa upinzani hadi kuwa cha kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani. Kakichukua kikiwa na wabunge watano (5) bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10 kina wabunge 49.
Ni ‘achievement’ kubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake CHADEMA imebeba ajenda nzito za kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa rasilimali, katiba mpya, nk.
Lakini kuna matatizo yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka huko mbele tunaweza kupata shida kubwa. Ni muhimu kwa Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake umefikia hapo asitake kulazimisha kusonga mbele akidhani bila yeye hakuna CHADEMA. Akiache chama kikiwa salama, abaki kama mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine awamu inayofuata ya kuingia madarakani.
Kama hataki kuwa mwelewa na kuachia ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao. Leo nitaainisha mambo machache tu yanayohusiana na fedha za chama na uaminifu ili wana-CHADEMA muelewe kwa nini viongozi wakuu wa chama wamehamaki sana kusikia wanatakiwa kuwasilisha ripoti za fedha wakajikuta wanapambana na mwenyekiti wa kamati ya bunge badala ya kamati na hata kufikia kusahau kwamba huyo mwenyekiti wa kamati ya bunge ni mwenzao, ni naibu katibu mkuu wa chama. Mengine nitaendelea kuyadondoa siku nyingine nitakapopata fursa:

Mabadiliko ya Katiba ya CHADEMA
Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa.
Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo, lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithilika kwa chama.
Ni muhimu wana-CHADEMA mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepo leo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi.
Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa kina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wana-CHADEMA hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu, bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.
2. Matumizi ya fedha za chama:
Hakuna mtu anayejua hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu. Maamuzi ya vikao hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010, vikao halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa, bali zitunzwe kwenye akaunti maalumu kwa ajili ya uchaguzi wa 2015.
Lakini leo si tu akaunti hiyo haina fedha, bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha. Watu watatu ndo wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya kikao cha Baraza Kuu cha Januari kilichoamua kwamba kiasi cha fedha kinachotoka serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya na majimbo na kiasi kingine kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa ipasavyo.
Nyinyi viongozi wa kanda, mikoa, wilaya na majimbo ni mashahidi wa hili. Lakini kuna michango ya watu binafsi kama Mzee Sabodo, hizo nazo hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje. Hapo sijataja fedha zinazopatikana kutoka kwenye ‘Fund-Raising Events’ mbalimbali kama ile ya Dar es Salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha hizo ‘Fund-Raising’, uaminifu wao kwenye masuala ya fedha ni ‘questionable’ (unatia wasiwasi).
3. Taarifa za fedha
Tokea baada ya uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi kupokea na kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za chama. Kila kikao ajenda hiyo inarushwa kiaina.
Wanaojua mchezo huo ni watu watatu hawa na malengo ya kurusha hiyo ajenda kila wakati na kukwepesha isijadiliwe pia wanayajua wao.
Ni dhahiri tukiendelea na hawa watatufikisha mwaka 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama.
4. Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama
Wakuu waliopo hawana hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya ‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya matukio.
Mawazo mazuri kama ya kuanzisha kampuni ya uwekezaji ya chama itakayowekeza kwenye miradi mbalimbali, haijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana.
Hatuwezi kufika hata siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa Kenya juzi juzi wakuu wetu ingawa walishiriki, lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.
5. Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi
Chama chetu kinayo kamati ya tenda ambayo iko chini ya sekretariati, lakini kamati hii haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda kwa kuwa ni dhaifu na wamekubali kuzimwa.
Leo ikidaiwa kamati hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, kadi za uanachama, seti ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa katibu mkuu, hawana. Manunuzi haya yote yanafanywa na wakuu bila utaratibu wowote, jambo ambalo ni hatari.
Hivi tunavyoongea, ni mwenyekiti taifa mwenyewe ndiye aliyenunua magari na pikipiki zote za M4C.
Hivi tunavyoongea kuna sh. milioni 80 ambazo alizichukua na kuagiza kadi za uanachama tangu mwaka jana mpaka leo hizo kadi hazijawahi kuonekana.

6. Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya uenezi vya chama
Hakuna kikao chochote cha juu kilichojadili au kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba sasa kuna mtu binafsi amepewa tenda ya kuuza vifaa vya chama na chama kinanufaika vipi na mauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya chama kama bendera vinauzwa na mtu binafsi.
Napenda kwanza kuipongeza kamati ya bunge kwa kuvikomalia vyama vinavyopokea ruzuku bila kujali ni chama tawala au upinzani.
Pili, namshauri CAG unaweza kutumia kampuni binafsi kwenye wizara, idara, taasisi, wakala na asasi zote za kiserikali na serikali za mitaa kwenye ukaguzi, lakini kamwe usiruhusu vyama vya siasa vikaguliwe na kampuni hizo.
Hapo nenda mwenyewe ndio utajionea mwenyewe. Kampuni binafsi kwenye vyama huko zinafundishwa ziandikeje maoni yao. Nenda mwenyewe ujionee.

Pia, kuna mkakati unaendeshwa na CHADEMA kwa sasa wa kuwapigia simu viongozi wa mikoa, hasa hapa Dar es Salaam na mikoa mikubwa kama Mwanza, Arusha, Mbeya nk, wakiwataka watoe matamko kumpinga Zitto. Kataeni ushenzi huu. Hili si jambo la Zitto ni la kamati ya bunge na kimsingi ni la uadilifu ndani ya serikali na vyama.
Hata kama jambo lenyewe lingekuwa limeagizwa na Mwigulu Nchemba msingetoa matamko ya kupinga zaidi ya kuwaacha viongozi wetu wakuu watoe ripoti kuthibitisha uadilifu wao, japo kidogo maana ni ukweli pia kwamba kwenye ripoti wanaweza kuzuga zikawa safi, lakini ufisadi umefanyika.
Kama ni matamko toeni matamko ya kuutaka uongozi wetu utoe hizo ripoti, na hapo ndipo mtakapojua kwa nini hampati ruzuku. Kuna matumizi mengi sana ya hovyo na ufisadi mkubwa unafanyika hapo Makao Makuu.
Nitaendelea kuwadondolea ili muone kwa nini napendekeza tuung’oe uongozi huu chini ya Mbowe.
Ahsanteni kwa kunisoma

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru