Tuesday 29 October 2013

Ngeleja azamisha jahazi la CHADEMA


NA PETER KATULANDA, SENGEREMA
VIJANA 38 wakiwemo wapiga debe wa daladala wa Kamanga Ferry, Kata ya Nyamatogo wilayani Sengerema, wametimka kutoka vyama vya CHADEMA na CUF na kujiunga na CCM.
Wamedai kuvutiwa na sera za Chama zilizotangazwa na Mbunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthon Diallo.
Walivihama vyama hivyo hivi karibuni na kuanzisha kikundi cha ujasiriamali cha Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), tawi la Kamanga, kwa madai kuwa wamechoshwa kutumiwa katika maandamano yasiyokuwa na tija, yenye lengo la kuwagawa Watanzania.
Wakizungumza katika kikao maalum cha maandalizi ya uzinduzi wa kikundi hicho juzi, walisema vyama hivyo vya upinzani vimejaa unafiki, ubinafsi na ubabaishaji ambao hautaweza kuwakomboa wananchi katika umaskini.
Walisema wanaimani kubwa na CCM kutokana na sera zake nzuri zikiwemo za kuwawezesha kiuchumi vijana, hivyo wamemuomba Ngeleja na Diallo wawawezesha kupata ‘boda boda’(pikipiki) za mikopo.
“Umaskini ndio unaotufanya tutange tange na kutumiwa hovyo kisiasa, lakini sasa tumejiunga na Chama Mama, kupitia UVCCM, tunaamini maisha yetu yataboreka.
“Tunamuomba mheshimiwa Diallo na Mbunge wetu Ngeleja, watusaidie kupata mikopo ya pikipiki,” alisema Nuhu Maulid, Mwenyekiti wa vijana hao.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyamatongo, Adam Yusuph, akiwapongeza vijana hao kwa kujiunga na CCM, alisema Chama kitahakikisha wanafikia maendeleo makubwa ya kiuchumi na kisiasa ili wawe mfano wa kuigwa na wengine waliosalia upinzani.
Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata hiyo, Said Manyasi, alisema vijana waliokikimbia CHADEMA na kujiunga na CCM katika tawi hilo, wanafikia 38.
Alisema sera ya CCM ni kulinda vijana na kuwapatia maendeleo, siyo kuwatumikisha.
Manyasi, aliwataka wakitumikie Chama kwa bidii na moyo mkunjufu na kuahidi kufikisha kilio chao kwa Ngeleja na Diallo na kutoa wito kwa UVCCM kuzingatia vikao vya kikatiba na kuhamasisha vijana wachape kazi na kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili wapewe mikopo.
Ngeleja, akizungumza na UHuru juzi, alisema anawapongeza vijana hao kujiunga na CCM.
Aliahidi kuwapa ushirikiana na viongozi wengine wa Chama, ili vijana hao na wajasiriamali wengine waliojiunga katika vikundi, wapate mikopo ya kuwakwamua kiuchumi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru