Tuesday 22 October 2013

JK: Ni fedheha serikali kudaiwa


na mwandishi wetu, njombe
RAIS Jakaya Kikwete, amesema ni aibu kwa serikali kudaiwa na wakulima.
Hivyo, amewahakikishia wakulima wilayani Ludewa, mkoa wa Njombe, kuwa watalipwa madai yao haraka iwezekanavyo.
Wakulima hao wanaidai serikali baada ya kuiuzia mahindi.
Aidha, Rais Kikwete, amethibitisha kuwa meli ambazo serikali yake iliahidi kununua kwa ajili ya usafiri katika maziwa makuu ya Tanzania, zinajengwa na zitazinduliwa kabla ya mwaka 2015.
Alisema meli hizo zitakuwa sita na zitagawiwa mbili mbli kwa maziwa matatu ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.
Rais Kikwete aliyasema hayo juzi alipozungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara.
Rais yuko katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani Njombe, ambapo pamoja na kukagua shughuli za maendeleo, amezindua miradi kadhaa na kuweka mawe ya msingi.
Rais Kikwete alikiri kuwa serikali inadaiwa sh. bilioni 17, na wakulima wa mikoa mbali mbali nchini, ambao waliiuzia mahindi msimu uliopita kupitia kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Rais Kikwete, aliambiwa hayo jana, alipokuwa akipokea ripoti ya Maendeleo ya wilaya ya Ludewa.
Katika ripoti aliyosomewa, ilidaiwa kuwa  wakulima wa wilaya hiyo pekee, wanaidai serikali sh.bilioni 3.115, ambayo ni thamani ya mahindi tani 6,231, ambayo wakulima hao waliiuzia NFRA.
Rais Kikwete aliambiwa kuwa mpaka sasa wakulima hao wamelipwa sh.bilioni 2.839 za tani 5,679 za mahindi.
NFRA ilikuwa imelenga kununua mahindi tani 13,000 toka kwa wakulima wa wilaya hiyo.
Hata hivyo, mpaka sasa imeweza kununua kununua tani 11,911, ingawa sehemu kubwa ya kiasi hicho hakijalipiwa na serikali.
“Hii ni aibu. Serikali haiwezi kudaiwa na wakulima. Hizi fedha zitalipwa tu,” alisema Rais Kikwete na kuelezea hatua ambazo amezichukua binafsi, katika siku mbili akiwa wilayani humo, kuhakikisha wakulima hao wanalipwa.
Rais Kikwete pia alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kununua tani 2,972 za mahindi ya msimu uliopita zilizobakia mikononi mwa wakulima wa wilaya hiyo.
“Naambiwa kuwa bado NFRA inahitaji kiasi cha tani 40,000 hivi, ili kukamilisha shehena ya tani 250,000 za mahindi kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa mwaka huu.
“Nitawaambia waangalie kama wanaweza kununua kiasi hiki kilichobakia mikononi mwa wakulima wa Ludewa.”
Kuhusu maombi ya wakazi wa Ludewa kununuliwa meli nyingine baada ya kuzama kwa Mv. Mbeya Ziwa Nyasa, Rais alisema meli hiyo iko njiani, wavute subira.
“Tunajua kuwa meli ya Mv. Mbeya ilizama, hata hivyo, meli hizi zimezama katika maziwa mengine makubwa ya Tanganyika na Victoria, na mimi kwenye kampeni niliahidi kuwa nitanunua meli moja kwa kila ziwa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tumeagiza meli tatu kutoka Korea Kusini. Zinajengwa. Tumeagiza meli nyingine tatu kutoka Denmark. Nazo zinajengwa. Hivyo, tunaweza kupata siyo meli moja bali meli mbili katika maziwa yote matatu.
“Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuzizindua meli hizo kabla ya kumaliza kipindi changu cha uongozi, mwaka 2015.”
Rais Kikwete pia alifafanua kuhusu kero nyingine zilizoibuliwa na wakazi hao, ikiwa ni pamoja na ya ujenzi wa daraja kwenye Mto Ruhuhu, ambapo aliahidi kuwa litajengwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru