Tuesday 22 October 2013

RC atishia kuachia ngazi


Na Theodos Mgomba, Dodoma.
MKUU wa mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi, amesema yuko tayari kuondoka mkoani hapa, lakini si kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara wakati wa vikao vya Bunge vikiendelea.
“Kama kwa kuzuia mikutano hiyo kutanifanya kuondoka Dodoma nipo tayari, lakini hii ni kwa maslahi ya taifa.”
Aliyasema hayo mjini hapa jana, wakati akijibu swali kuhusiana na marufuku iliyowekwa ya kufanyika kwa mikutano ya hadhara wakati wa vikao vya Bunge.
Dk. Rehema, alisema ametamka wazi bila kupindisha maneno wala kumung’unya.
Aliswema kuna baadhi ya vyama, huamua kufanya makusudi kuandaa mikutano mjini humo, wakati vikao vya bunge vikiendelea, jambo ambalo huwaletea usumbufu.
“Na kuna baadhi huamua tu kujipangia mikutano hiyo ghafla tu, ili mradi kuna jambo hawakulipenda limetamkwa bungeni, basi hukimbilia kutaka kufanya mikutano ya hadhara ambayo wakati mwingine hujaa maeneo ya uchochezi,” alisema Dk. Rehema.
Alisema agizo hilo linavihusu vyama vyote vya siasa.
“Kwanza idadi ya askari wanaokuwepo wakati wa Bunge, hailingani na idadi ya watu wanaokuja mkoani hapa,” alisema.
Alisema kuruhusu kufanyika kwa mikutano hiyo ya hadhara, kunaweza kupunguza nguvu ya ulinzi.
Kauli hiyo ya Dk. Rehema, imekujja baada ya Katibu wa CHADEMA mkoa wa Dodoma, Stephen Masawe, kuuliza ni kwanini vyama vya siasa vinazuiwa kufanya mikutano yake wakati wa vikao vya Bunge.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru