Tuesday 22 October 2013

Kanisa lachomwa, muumini auawa


Na waandishi wetu, Dar na Mwanza
WATU wasiojulikana wamevamia na kulichoma moto Kanisa la Baptist lililopo Vingunguti, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8.20 usiku, eneo la Faru, mtaa wa Mtambani na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo.
Alisema watu wasiofahamika walionekana katika eneo hilo ambapo inadaiwa ndiyo waliowasha moto huo uliounguza mazabahu ya kanisa hilo.
Marietha, alisema nyuma ya kanisa kuna nyumba ya Mchungaji, Hezron Mwaisemba na binti wa nyumba ya jirani aliyekuwa ametoka nje usiku huo kujisaidia, ndiye aliyewaona vijana hao wakitokomea.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, moto ulizimwa na wakazi wa eneo hilo na haukuwa na madhara kwa binadamu.
Alisema vijana hao wanadaiwa walikuwa na chupa ya mafuta ya petroli ambayo waliyatumia kuchoma kanisa hilo.
Katika tukio lingine, muumini wa Kanisa la Gilgal Christian Worship Centre lililopo Ilemela jijini Mwanza, ameuawa kwa kucharangwa na mapanga na wengine wawili kujeruhiwa.
Tukio hilo lilitokea baada ya watu wasiofahamika kuvamia kanisani hapo wakati wa mkesha wa maombi saa 7:00 usiku wa kuamkia jana.
Askofu wa Kanisa hilo, Eliabu Sentoz, alimtaja aliyeuawa kuwa ni Elia Meshack na waliojeruhiwa ni Elias Msakuzi na Tumsifu Pungu, ambaye amelazwa Hospitali ya Rufani Bugando.
“Ni kweli waumini wetu watatu waliokuwa kwenye mkesha wa maombi, walivamiwa, mwenzao mmoja aliyekuwa mlango wa nyuma akiwalinda wenzake wakati wanaendelea na maombi ameuawa,’’ alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru