Tuesday 1 October 2013

Wakurugenzi mtegoni


Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais, Dk. Mohammed Ghalib Bilal, amewaagiza wakurugenzi wa majiji, miji na halmashauri za wilaya nchini kuhakikisha wanateua waratibu watakaohusika kusimamia upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee bila ya kuwepo kwa vikwazo vya aina yeyote ile kwa jamii hiyo.
Wakati Dk. Bilal akitoa maagizo hayo, Naibu Waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanry amesema hadi mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu, halmashauri zote zitakazokuwa hazijakamilisha utaratibu wa vitambulisho utakaowawezesha wazee kupata huduma za afya kwa uhakika wakurugenzi wake watawajibishwa.
Ujumbe huo ulitoka kwa viongozi hao juzi, walipokuwa kwenye kilele cha siku ya maadhimisho ya siku ya wazee duniani ambayo kitaifa ilifanyika wilayani Korogwe ambapo mgeni rasmi alikuwa Dk. Bilal ambaye alisema kwamba serikali inatambua changamoto za wazee, huku hatua kadhaa zikiwa zimeanza kuzichukua.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Bilal alisema tayari serikali imeviagiza vituo vyote vya afya kuhakikisha vinatenga madirisha maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wazee kwa madai kuwa, kada hiyo inapaswa kuheshimiwa kutokana na mchango wake kuwa muhimu katika maendeleo ya nchi ambapo hatua za makusudi zitachukuliwa kuwaimarishia usalama.
Kutokana na hali hiyo Dk. Bilal alisema, halmashauri za wilaya,miji na majiji wakurugenzi wake wanahitajika kuharakisha maandalizi ya vitambulisho vya wazee vitakavyowarahisishia upatikanaji wa afya kwa uhakika njia ambayo itawawezesha kuwa na afya bora, huku akiwahimiza watendaji hao kutafuta waratibu wa mpango huo.
“Serikali inathamini mchango wa wazee katika maendeleo nchini, hivyo katika afya nawaagiza wakurugenzi wa majiji, miji na halmashauri kuhakikisha watateua waratibu watakaosimamia upatikanaji wa huduma za afya kwa wazee bila ya kuwepo kwa kikwazo cha aina yoyote, Comrade Mwanri ameshasema atapita kule,” alisema Dk. Bilal.
Licha ya Dk. Bilal kuhimiza umuhimu wa mazingira ya upatikanaji wa afya kuboreshwa kwa kada ya wazee, hususan uwepo wa dirisha maalumu la kuihudumia kada hiyo, pia alisema watu wote wanawajibika kuona kuwa wazee wanakuwa naamani, wanaishi maisha bora na kuheshimika mambo ambayo yanapaswa kuasisiwa na jamii nzima.
Aidha, alitilia msisitizo umuhimu wa kuwakemea watu wote wenye nia mbaya ya kueneza chuki ili kuweza kujipatia maslahi binafsi, akisema kuwa watu wa aina hiyo lazima waeleweke kuwa hawana nia njema na Taifa hili ila lengo lao kuu ni kuhatarisha ama kuvunja umoja wa Tanzania vitendo ambavyo havitavumiliwa kujitokeza.
Alisema serikali itaendelea kupambana na vitendo vyote vyenye kuashiria kuvunjika kwa hali ya usalama na amani, hasa kwa kada ya wazee ambapo amevikumbusha vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinatekeleza wajibu wao ipasavyo ili kudhibiti vitendo ambavyo vinahatarisha usalama nchini Tanzania.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema serikali itahakikisha kwamba katika bunge lijalo inajitahidi kuangalia uwezekano wa kuwasilisha hoja ya sheria za wazee hatua ambayo itawezesha kada hiyo kupata mahitaji yake pasipo kutegemea mashinikizo ya viongozi, jambo ambalo alisema lilikuwa lijadiliwe kipindi kilichopita.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa akizungumza kabla ya Makamu wa Rais kuzungumza na wazee wa maeneo mbalimbali nchini, aliwataka wahusika kuwa wa kwanza kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu wanaojihusiaha na vitendo vinavyohatarisha usalama, hususan utaratibu wa baadhi ya waganga wa jadi kupiga ramli.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru