Thursday 24 October 2013

Madudu yafichuka daraja la Rusumo



Na Alphonce Kabilondo, Ngara
UJENZI wa daraja la mto Rusumo linalounganisha Tanzania na Rwanda, umeghubikwa na madudu baada ya kubainika kutokuwa na mlinganyo wa viwango vya miundombinu kati ya nchi hizo mbili.
Hilo lilibainika wakati Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli, alipotembelea mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Japan kwa lengo la kukuza uchumi katika nchi wanachama wa Afrika Mashariki.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi ya Dk. Magufuli iliyowahusisha pia Mwakilishi wa Waziri wa Ujenzi wa Rwanda pamoja na Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, ilibainika kuwepo kwa mapungufu ambayo yametokana na baadhi ya wataalamu wa serikali ya Tanzania kushindwa kutoa ushauri wenye manufaa kwa nchi.
Ilibainika kuwa ofisi za idara, urefu wa barabara ya lami kufika kwenye daraja,, kituo kikubwa cha kupaki magari na mizigo vikiwa upande wa Rwanda huku Tanzania ikiwa na miundombinu michache, hatua inayotajwa inaweza kuathiri uchumi wa taifa huku ule wa Rwanda ukinyanyuka.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Magufuli, alisema licha ya ujenzi huo kugharamiwa na Japan kwa aslimia 100, hakuna mlinganyo wa miundombinu na kwamba, hilo lazima liangaliwe kwa umakini wake.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi huo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, John Kalupale, alisema ujenzi huo umekamilika kwa asilimia 60, ambapo upande wa Tanzania umetekelezwa kwa asilimia 25 huku Rwanda ukiwa umefikia asilimia 35 na uko chini ya Kampuni ya Daiho Corporations ya nchini Japan.
Kwa upande wake Balozi Okada, aliwatupia lawama baadhi ya watendaji wa serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuishauri serikali yao mapema juu ya ujenzi wa daraja hilo na kwamba, walipaswa kuwasilisha maoni kabla ya ujenzi kuanza



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru