Thursday 24 October 2013

Spika amwaga siri za wabunge





Na Mwandishi Wetu
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amemwaga hadharani kuwa baadhi ya wabunge waliomaliza muda wao, wana hali ngumu kimaisha na wengine huenda ofisi za Bunge kulia hali ili wapatiwe msaada.
Alisema kufuatia hali hiyo, Bunge linajipanga kuanzisha na kutekeleza mikakati mbalimbali ili wawezesha kuondokana na fedheha hiyo mbele ya jamii.

Spika Anne, alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni kuanzisha mafunzo maalumu ya ujasiriamali kwa wabunge waliopo madarakani kwa lengo la kuwanusuru ili wasikumbane na hali kama za watangulizi wao.
Alisema karibu kila siku anapata ugeni wa wabunge wa zamani wanaofika ofisini kwake kuomba msaada.
Spika Anne, ambaye ni mbunge wa Njombe Kaskazini (CCM), aliyasema hayo jana, Ofisi Ndogo za Bunge mjini Dar es Salaam, alipokutana na Spika wa Bunge la Uswisi, Maya Graf, aliyefika kumtembelea.
Alisema baada ya kuwa Spika wa Bunge, amebaini wabunge wengi wanaomaliza muda wao wana maisha magumu huku wachache ndio wenye uwezo wa kujikimu.
“Nilipochaguliwa kuwa Spika nimeona mambo mengi, baadhi ya wabunge wanaomaliza muda wao wanakuwa na hali mbaya ya kimaisha.
“Kuna siku ofisini kwangu walikuja wabunge watano kutaka msaada na sikuwa na uwezo wa kuwasaidia wote kwa wakati huo, nikalazimika kuwapa nusu wengine walilalamika,” alisema.
Kwa mujibu wa Spika Anne, kutokana na hali hiyo, Bunge limedhamiria kuandaa mafunzo maalumu ya ujasiriamali na kwamba, yatatolewa kwa wabunge waliopo bungeni hivi sasa.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo ili watakapomaliza vipindi vyao vya ubunge, wasiyumbe kimaisha na yatakuwa ya hiari.
Alisema wakati wa mfumo wa chama kimoja, kulikuwa na utaratibu wa kuwapa pensheni wabunge, lakini baada ya mfumo wa vyama vingi, utaratibu huo ulifutwa.
Alisema ifike wakati, jamii isiigeuze siasa kuwa kazi ya kudumu na kwamba, hali hiyo inasababisha uchaguzi wa Tanzania kuwa mgumu.
Aliongeza kuwa mishahara ya wabunge wa Tanzania ni midogo ukilinganisha na ya nchi zingine.
Kwa upande wake, Maya, alisema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali ya Uswisi hapa nchini.



Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru