Wednesday 30 October 2013

Mkono uliokuwa ukiuzwa mtaani


ni wa mwanafunzi
NA PETER KATULANDA, MWANZA
MKONO wa binadamu, ambao walikamatwa nao watu watatu, wakiwemo waganga wa kienyeji wawili na mfanyabiashara mmoja, umebainika kuwa wa kijana wa miaka 11 (jina linahifadhiwa), ambaye kwa sasa amelazwa akipatiwa matibabu.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, kijana huyo alikatwa mkono wakati akijaribu kumuokoa mama yake mzazi walipovamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwao.
Oktoba 24, mwaka huu, watu wasiojulikana walimvamia mama wa kijana huyo, Dotto Luchagula (60) na kumshambulia kwa mapanga hadi kufa kwa kile kilichodaiwa imani za kishirikiana, ambapo mwanaye huyo alijaribu kupambana ili kumwokoa ndipo naye akakatwa kiungo hicho.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa, Joseph Konyo, alisema kijana huyo alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kongolo iliyopo wilayani Magu.
“Kijana huyu alikatwa mkono wake wa kulia wakati akijaribu kumuokoa mama yake aliyevamiwa na kuuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga nyumbani kwake Kijiji cha Kongolo katika Kata ya Nyabusu wilayani Magu,” alisema.
Aliongeza kuwa hadi jana jioni, kijana huyo alikuwa bado amelazwa hospitalini (jina linahifadhiwa kwa usalama wake zaidi) akipatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Watuhumiwa hao walitiwa mbaroni juzi, saa tisa alasiri, katika eneo la kati ya ufukwe wa Ziwa Victoria na Uwanja wa Ndege wa Mwanza, wakiwa kwenye harakati za kukiuza kiungo hicho kwa gharama ya sh. milioni 100.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru