Tuesday 8 October 2013

Makuti yaua mtoto


NA JUMANNE GUDE
WATU wawili wamekufa jijini Dar es Salaam katika matukio tofauti, likiwemo la mwanafunzi wa chekechekea Abdallah Ally aliyenaswa na makuti ya mnazi shingoni.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kinondoni, Camilius Wambura alisema tukio hilo lilitokea juzi, saa 10.20 jioni, maeneo ya Mwananyamala Bwawani.
Wambura alisema Ally na watoto wenzake walikuwa wanacheza, ambapo inasadikiwa alipanda juu ya matairi yaliochimbiwa chini ya mnazi kwa lengo la kubembea.
Alisema wakati anabembea, ghafla alinaswa na makuti shingoni ambayo yalikuwa yamefungwa kwenye mnazi na kumsababishia kifo.
Aidha, Wambura alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, huku upelelezi unaendelea.
Katika tukio lingine, Salum Malegera amekufa baada ya kuanguka ghafla, maeneo ya Tandika Maguruwe, wilayani Temeke.
Kamanda wa Polisi Mkoa Temeke, Englebert Kiondo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, juzi, saa 3.45 asubuhi, katika eneo hilo ambapo, Malegera alianguka na kufariki papo hapo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru