Thursday 24 October 2013

Serikali yaibana Barrick




NA SELINA WILSON
SERIKALI imeiagiza Kampuni ya uchimbaji madini ya African Barrick, kutekeleza ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa barabara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mkutano wa pamoja kati ya wachimbaji wadodo, wakubwa na serikali, mjini Dar es Salaam.
Masele, alisema kuna ahadi nyingi zilizoahidiwa na kampuni hiyo ambazo baadhi zimetekelezwa na zingine hazijatekelezwa.
Hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inazitekeleza haraka iwezekanavyo.
Alitaja baadhi ya ahadi hizo kuwa ni ujenzi wa shule, ununuzi wa madawati kwa shule za msingi, kuchimba visima katika vijiji saba na kusomesha vijana hadi chuo kikuu, ambazo alisema baadhi zimetekelezwa na zingine bado.
Masele, aliwahakikishia wakazi wa eneo hilo, kuwa serikali itafuatilia na kusimamia kikamilifu ili ahadi za barabara na maji zitekelezwe kwa lengo la kuboresha huduma za jamii kwa wananchi walioko jirani na migodi.
Kuhusu mkutano huo wa mkakati wa pamoja (MSP), alisema unalenga kuanza utekelezaji wa mradi wa kuwezesha wachimbaji wadogo katika maeneo ya Mgusu mkoani Geita na Tarime mkoani Mara.
Alisema chini ya mradi huo wenye lengo la kuondoa migogoro, wachimbaji wadogo watawezeshwa kwa kupatiwa utaalamu na vifaa vya uchimbaji wa kisasa badala ya kuchimba kiholela.
Masele, alisema wachimbaji wadogo watakaonufaika na mradi huo ni wale waliopatiwa leseni za uchimbaji.
Pia, watanufaika na mradi mkakati mwingine wa serikali wa kuwawezesha kwa mikopo kwa ajili ya vifaa na mitaji itakayotolewa na benki ya TIB.
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa shirikisho la wachimbaji wadogo, John Bina, alisema haipendezi kuona kampuni kubwa zikichimba madini na kuondoka huku jamii ikibaki bila kunufaika.
Alisema utaratibu huu wa wachimbaji wadogo ambao ndio wenyeji, wataanza kuona matunda.
Bina, alisema serikali imefanikiwa kuondoa migogoro kati ya pande hizo mbili, kwa kuunda ushirikiano na kuhusisha Benki ya Dunia (WB) pamoja na wadau wengine muhimu, kukaa pamoja na kutoka na mkakati huo.
Kwa upande wake Meneja wa Uendelezaji Endelevu wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti, Rebecca Steven, alisema mradi huo utatoa matokeo chanya na manufaa makubwa.
Rebecca alisema pia mkutano huo utatoka na mpango wa utekelezaji wa namna kampuni zitakavyowasaidia wachimbaji wadogo.
Migogoro baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo wa madini hapa nchini, imedumu kwa muda mrefu, ambapo kilio cha wachimbaji wadogo ni kutokuthaminiwa na wakubwa na kuondolewa katika maeneo yao.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru