Tuesday 1 October 2013

Sheikh Ponda agonga mwamba


Na Latifa Ganzel, Morogoro
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa, imetupilia mbali ombi la Katibu wa Jumuia na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa, la kutaka kufutiwa shitaka moja ya mashitaka yanayomkabili.
Wakati Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Richard Kabate, akitoa uamuzi huo, Sheikh Ponda, aliwakana mawakili wawili kati ya watatu waliojitokeza kumtetea.
Hakimu Kabate alitupilia mbali maombi yaliyowasilishwa Septemba 17, mwaka huu na Wakili Juma Nassoro, aliyekuwa akimwakilisha Sheikh Ponda, ya kuomba mahakama kufuta shitaka la kukiuka amri iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyomtaka ndani ya mwaka mmoja awe anahubiri amani.
Katika maombi yake, Nassoro alitaka shitaka hilo lifutwe au lirudishwe Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam ilipotolewa hukumu.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Kabate alisema mshitakiwa anadaiwa kutenda makosa katika eneo la Kiwanja cha Ndege mjini hapa, hivyo hawezi kushitakiwa Dar es Salaam.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, jana Sheikh Ponda ambaye alikuwa akiwakilishwa na Wakili Yahaya Njama kwa niaba ya Nassoro, aliwakana mawakili wawili. Mawakili hao ni Ignas Punge na Bathlomeo Tarimo.
Hali hiyo ya kuwakana ilikuja baada ya mawakili wote, akiwemo Nasoro kutofika mahakamani wakati kesi yake ikisilizwa na kuwakilishwa na Wakili Njama aliyekuwa akimtetea katika kesi ya awali katika Mahakama ya Kisutu.
Awali, Wakili Njama, alidai anamwakilisha Wakili Nasoro kwa kuwa yuko nchini India akipatiwa matibabu ya macho na atarejea nchini baada ya afya yake kutengemaa katika kipindi cha mwezi mmoja.
Hali ya kukanwa kwa mawakili hao, ilijitokeza wakati wa kupangwa kwa tarehe ya usikilizwaji wa shauri hilo Novemba 7, mwaka huu, ambapo Wakili wa Serikali, Benard Kongola, aliutaka upande wa utetezi kutokuwa na kikwazo cha tarehe kwa kuwa kutambua mshitakiwa anatetewa na mawakili Punge, Tarimo na Nasoro.
Baada ya Kongola kudai hayo, wakili Njama alidai hawatambui mawakili wengine zaidi ya Nasoro ambaye alimwagiza amwakilishe kwenye kesi hiyo.
Alipowasikiliza hoja za pande zote husika, Hakimu Kabate alitoa barua ya wakili Tarimo, ambaye aliomba udhuru wa kutofika mahakamani kwa siku hiyo.
Hakimu Kabate alisema yeye anawatambua mawakili hao kwa kuwa wamekuwa wakishiriki mwenendo wa kesi hiyo, na tayari kuna kumbukumbu za maandishi mahakamani hapo, na kwamba iwapo wamejitoa walitakiwa kutoa taarifa kwa maandishi.
Kutokana na hilo, Wakili Njama aliomba mahakama iwape muda na kwamba watalishughulikia suala hilo na kupeleka taarifa sahihi mahakamani.
Mshitakiwa alirudishwa rumande hadi Novemba 7, mwaka huu, kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.  Oktoba 15, mwaka huu, kesi itatajwa bila mshitakiwa kufika mahakamani.
Sheikh Ponda anakabiliwa na mashitaka matatu, yakiwemo ya uchochezi na la kukiuka amri ya Mahakama ya Kisutu.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Agosti 10, mwaka huu, katika eneo la Kiwanja cha Ndege mjini hapa. Mshitakiwa huyo anadaiwa kuwaambia Waislamu kwamba:
ìNdugu Waislamu msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti, kwani kamati hizo zimeundwa na BAKWATA ambao ni vibaraka wa CCM na serikali, na kama watajitokeza kwenu watu hao na wakajitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi  na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.î
Inadaiwa kauli iliumiza imani za watu, pia ni kinyume cha agizo la Mahakama  ya Kisutu, Dar es Salaam, lililotolewa na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Mei 9, mwaka huu, ambayo ilimtaka ndani ya mwaka kuhubiri amani.
Shitaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kutoa maneno yenye nia ya kuumiza imani za dini nyingine kwa kuwaambia Waislamu kwamba:
“Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka, na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.”


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru