Thursday, 13 November 2014

Escrow kaa la motoNA THEODOS MGOMBA, DODOMA
KASHFA ya madai ya kuchotwa mabilioni ya shilingi kwenye akaunti ya ESCROW, imezidi kuwa moto kutokana na kuibua mjadala mkali bungeni kila kukicha.
Tayari serikali iliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini iwapo malipo hayo kwa Kampuni ya PAP, iliyonunua IPTL, yalifanyika kihalali, ambapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imepewa jukumu hilo.
Hata hivyo, habari za kuaminika zinasema kuwa, mbali na watendaji wa serikali, baadhi ya wanasiasa wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani na wabunge, ni miongoni mwa wanaodaiwa kunufaika na mabilioni hayo kila mmoja kwa namna yake.
Kwa upande wa wanasiasa, taarifa zinasema yumo mbunge wa upinzani, aliyechota kiasi cha sh. bilioni 20 kama mgawo, ambapo kwa sasa amekuwa na wakati mgumu kutokana na ukimya wake kutiliwa shaka na wanasiasa wenzake.
Hivi karibuni, ilielezwa kuwa taarifa ya uchunguzi huo itakabidhiwa kwa mamlaka husika muda wowote na kwamba, iko kwenye hatua za mwisho huku taarifa zingine zikidai kuwa imeshakamilika.
Tangu kuanza kwa Bunge, hoja kuhusu taarifa hiyo ya uchunguzi wa akaunti ya ESCROW, imekuwa ikizuka kwa wabunge kuhoji ni lini itawasilishwa, ambapo serikali hutoa majibu, lakini jana ikaibuka tena.
Baadhi ya wabunge walitaka Bunge kuiagiza serikali kuwasilisha taarifa hiyo ili ijadiliwe kwa kina, ambapo Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisimama na kuwaeleza kuwa TAKUKURU haiwajibiki kupeleka taarifa yake ya uchunguzi Bungeni.
Alisema hakuna kitu ambacho kitafichwa kuhusiana na sakata hilo na kwamba, taarifa zote za uchunguzi zitakazobainika, zitawekwa hadharani kwa maslahi ya taifa.
Ndugai alisema taarifa ya uchunguzi kuhusiana na sakata la akunti ya Escrow, itakayowasilishwa bungeni ni ile itakayowasilishwa na CAG wakati ya TAKUKURU itawasilishwa kwa mamlaka zingine, ikiwemo Ofisi ya Mwendesha Mashitaka wa Serikali (DPP) kwa hatua zaidi za kisheria.
‘’Kwa kawaida taarifa hizo zikija bungeni, haziwasilishwi moja kwa moja ndani ya Bunge bali zinapitia katika kamati husika na kamwe TAKUKURU haiwajibiki kuleta taarifa yake kwetu,” alisema Ndugai.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Wizara Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, alisema serikali itaangalia namna itakavyofaa ili taarifa ya TAKUKURU iwasilishwe bungeni bila kuathiri uchunguzi wake. 
Awali, baadhi ya wabunge walilitaka Bunge kuiagiza TAKUKURU kutoa taarifa ya uchunguzi wake kuhusiana na akaunti Escrow kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuomba mwongozo wa Naibu Spika, wabunge hao walisema pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kukabidhi taarifa yake kwenye kamati hiyo, pia TAKUKURU hawana ujanja wa kutokabidhi taarifa yake.
Akiomba mwongozo wa Spika, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, alisema pamoja na kamati yake kupatiwa taarifa ya CAG, bado inahitaji taarifa zaidi kutoka TAKUKURU.
‘’Tuna changamoto kuwa pamoja na taarifa ya CAG, ili kamati yangu iweze kufanya kazi yake vizuri, taarifa ya TAKUKURU iwepo,” alisema.
Alisema kumekuwa na minong’ono mingi kati ya wabunge juu ya watu wanaohusishwa na fedha kwenye akaunti ya Escrow, hivyo ili kuondoa giza hilo ni muhimu jambo hilo likawekwa wazi.
‘’Tunakuomba uiagize serikali kuileta taarifa ya TAKUKURU ili tuwe na taarifa zote mbili kwa pamoja na mchakato mzima uwe wazi.
‘’Wabunge wenzangu mimi najua mnapitiwapitiwa huko, hivyo mchakato mzima uwe wa wazi na kila mtu ahukumiwe kwa kile alichofanya,’’ alisema Zitto.
Mbunge achota bil.20/-
Wakati wabunge wakipambana kuhakikisha taarifa ya uchunguzi wa akaunti ya Escrow inawekwa wazi, taarifa zinadai kuwa mbunge mmoja (jina linahifadhiwa), anadaiwa kuwa miongoni mwa waliochota fedha hizo.
Habari kutoka kwenye chanzo chetu zinadai kuwa, mbunge huyo, ambaye ni mahiri wa kupiga kelele bungeni, amevuta mabilioni hayo kwa malengo ambayo hayajafahamika mpaka sasa.
Imedaiwa kuwa mbunge huyo kutoka kwenye chama cha upinzani, kwa sasa amekuwa kimya tangu kuanza kurindima kwa sakata hilo, jambo ambalo limewafanya baadhi ya wanasiasa wenzake kutilia shaka ukimya wake.
Hata hivyo, kumekuwepo na orodha ndefu inayotolewa kwenye mitandao, ikihusisha baadhi ya watendaji na wanasiasa, wakiwemo wa vyama vya upinzani, kudaiwa kuhusika kwenye kupata mgawo wa mamilioni ya shilingi ya fedha za Escrow.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru