NA
CLARENCE CHILUMBA, MASASI
JESHI la Polisi mkoani
Mtwara, linawashilkilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na mabomu 18 ya
kutengenezwa kwa kutumia vifaa hatari vya kupasulia miamba.
Habari za kuaminika
zinasema watuhumiwa hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kutokana na kuishi
maeneo tofauti. Pia walinaswa na nyaya na unga maalumu ambao ni malighafi
zinazotumika katika kutengeneza mabomu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mtwara, Augustino Ullomi, alisema watuhumiwa hao walitiwa mbaroni mapema wiki
hii, ambapo kila mmoja alikutwa akiwa nyumbani kwake.
Alisema watuhumiwa wote
walikutwa na mabomu hayo wakiwa wameyahifadhi na kuwa kukamatwa kwao
kumefanikishwa na raia wema.
Kamanda Ullomi aliwataja watuhumiwa
hao kuwa ni Abdallah Hamisi (25) na Kibode Dua (37).
Alisema mtuhumiwa wa
kwanza kutiwa mbaroni alikuwa Abdallah, ambaye baada ya kubanwa alieleza yalipo
mabomu hayo na kuwa aliyapata kutoka Nanyumbu kwa Dua.
Kamanda Ullomi alisema
askari walikwenda na mtuhumiwa huyo nyumbani kwa Dua na kufanikiwa kunasa
mabomu mengine 17, barua, unga na nyaya zinazotumika katika utengenezaji wa
mabomu hayo.
Kwa mujibu wa Kamanda
Ullomi, watuhumiwa hao walipohojiwa zaidi, walidai waliyapata Tunduru mkoani
Ruvuma na mengine Nachingwea mkoani Lindi.
Aliongeza kuwa baada ya
uchunguzi kwa kushirikiana na wataalamu wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu,
walibaini mabomu hayo ni hatari na yana uwezo wa kuuawa watu wengi kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa Kamanda
Ullomi, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi
kukamilika.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru