Thursday 13 November 2014

Kesi ya vigogo TPA kusikilizwa Desemba


NA FURAHA OMARY
KESI ya matumizi mabaya ya madaraka, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe na Naibu wake, Hamad Koshuma, imepangwa kuanza kusikilizwa Desemba 2, mwaka huu. 
Mgawe na mwenzake, wanadaiwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Contruction, bila ya kutangaza zabuni. 
Washitakiwa hao walipanda kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mmbando. 
Mwendesha Mashitaka, Jackson Chidunda alidai shauri linakuja kwa  ajili ya kuanza kusikilizwa. 
Hata hivyo, Hakimu Augustina aliahirisha shauri hilo kwa kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Arufani Isaya, anayesikiliza shauri hilo hakuwepo. 
Hakimu Augustina aliahirisha shauri hilo hadi Desemba 2, mwaka huu, kwa kuanza kusikilizwa. 
Washitakiwa hao wanadaiwa  Desemba 5, 2011, katika Mamlaka ya Bandari Tanzania, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa na mamlaka hiyo, kama mkurugenzi mkuu na naibu mkurugenzi mkuu, katika utekelezaji wa majukumu yao, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutia saini mkataba wa biashara kati ya TPA na kampuni hiyo ya China. 
Inadaiwa  mkataba huo ulikuwa ni wa upanuzi wa gati namba 13 na 14 katika bandari hiyo, ambapo walifanya hivyo bila kutangaza zabuni, jambo ambalo ni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma. 
Inadaiwa  kitendo hicho kililenga kuipatia faida kampuni hiyo ya China.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru