Thursday 13 November 2014

Wananchi wagoma kuchangia maabara


NA EVA-SWEET MUSIBA,TARIME
WANANCHI wa Kata ya Matongo-Nyamongo, wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wamekataa kuchangia fedha za ujenzi wa maabara  kwa madai kuwa, fedha zao za maendeleo ya kata hazijalipwa kutoka mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara.
Akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Madiwani, Mtendaji wa Kata ya Matongo, Chacha Muniko, alisema wananchi wamekataa kuchangia fedha hizo kutokana na kuudai mgodi huo asilimia tano, ambayo ni sawa na sh. milioni 700.
Hata hivyo, taarifa hiyo ilikataliwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime, Nyanja Maiga, na kumtaka mtendaji huyo kutoka nje ya ukumbi.
Kauli hiyo ilizua  tafrani kubwa katika kikao hicho, ambapo madiwani wote walimtetea mtendaji huyo na kumtaka mkurugenzi  awajibike na si mtendaji wa kata hiyo.
Tafrani hiyo iliwekwa sawa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewele, ambaye alisema ofisi yake ilishugulikia madai hayo na kwamba, taarifa itatolewa kwa madiwani baada ya kukamilisha mazungumzo kati ya serikali na mgodi huo ili waweze kulipa deni hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Diwani wa kata hiyo, Machage  Bathromew, alisema wapo baadhi ya wenyeviti wa vitongoji wanachangia kuwafanya wananchi kugomea michango hiyo kwa madai kuwa serikali imeleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa maabara za sekondari.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru