NA SARAH ONESMO, MWANZA
HALMASHAURI ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, imepokea vifaa vipya vya afya na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Msaada huo umetolewa na Taasisi ya Grena Youth Production School (GYPS) ya Denmark na utaihusu Kata ya Nyanguge, ambako tayari vifaa hivyo vimekabidhiwa kwa uongozi.
Vifaa hivyo ni robota moja ya mashuka ya wagonjwa, nguo za madaktari na wauguzi, mashine ya utrasound, mashine moja ya EKG ya kupimia wagonjwa wa moyo na kompyuta 95.
Akizungumza na wananchi, Diwani wa Kata ya Nyanguge, Hilali Elisha, alisema lengo la kutafuta wadau na wafadhili mbalimbali ni kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.
“Mashine hizi zilizotolewa, zitasaidia wanawake wajawazito kufanyiwa uchunguzi, ambao utakuwa wa uhakika na kupewa majibu, lakini wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo pia watapimwa na kupata dawa,”alisema.
Aliongeza kuwa kompyuta 95 zilizotolewa na taasisi hiyo, zitapelekwa katika shule za msingi na sekondari, makanisa, Chuo cha Maendeleo cha Nyanguge , Ofisi ya Ofisa Tarafa ya Kahangara pamoja na kituo cha Polisi Nyagunge.
“Pamoja na wapinzani kupiga kelele, lakini CCM inaendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi na kuhakikisha kero na matatizo ya wananchi yanatafutiwa ufumbuzi wa haraka ili huduma za jamii ziweze kupatikana katika maeneo mbalimbali hapa nchini,”alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jackiline Liana, alimpongeza diwani huyo kwa juhudi zake za kuwaletea wananchi wa kata yake maendeleo na kuwataka wanasiasa kuiga mfano huo na si kupiga kelele jukwaani bila kuonyesha vitendo.
“Vifaa hivyo vitasaidia upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa afya kwa wananchi na pia wanafunzi watapata maarifa kwa kutumia teknolojia ya kompyuta kwa vitendo na kuongeza weledi wawapo shuleni,” alisema.
Alisema diwani huyo anatekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo na amekuwa msitari wa mbele kuhakikisha kero na matatizo ya kijamii yanatafutiwa ufumbuzi wa haraka, pia huduma kwa wananchi zinapatikana.
Mganga wa Kituo cha Afya cha Nyanguge, Innocent Charles, alisema pamoja na kituo hicho kupata mashine hizo, hakuna wataalamu wa kuzitumia, hivyo alimuomba diwani huyo kupeleka ombi la kupata wataalamu wa kuzitumia.
Thursday, 13 November 2014
Halmashauri Magu yapigwa jeki
07:07
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru