Thursday, 13 November 2014

Ndugai alalamikia mauaji ya wakulima Kiteto


THEODOS MGOMBA 

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai
 NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema amesikitishwa na mauaji ya wakulima yanayoendelea kutokea katika wilaya ya Kiteto,   ambayo inapakana na jimbo lake la Kongwa na kuitaka serikali kuingilia kati.Ndugai alifikia hatua hiyo jana baada ya Mozza Abeid  (Viti Maalumu-CUF) kuomba mwongozo wa Spika. 
Akitumia kanuni ya 68(7), Moza alisema kumekuwa kukitokea mauaji ya kutisha ya wakulima katika wilaya ya Kiteto. 
Moza alisema katika kipindi cha mwaka huu, zaidi ya wakulima 30 wameuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa. 
“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mwongozo wako, huko Kiteto yamekuwa yakitokea mauaji, ambayo yanaendelea siku hadi siku. Watu wenye silaha za jadi wamekuwa wakivamia familia za wakulima na kuwaua bila uwoga huku serikali ikiwa kimya. Nini maana yake?’’ Alihoji mbunge huyo. 
Akiwa amekerwa na jambo hilo, Naibu Spika alisema anasikitishwa na mauaji yanayoendelea katika eneo hilo. 
“ Sisi watu wa Kongwa tumeshamuachia Mungu mambo haya. Watu wanauawa hovyo kama vile siyo Tanzania,” alisema. 
Naibu Spika alisema mauaji hayo yamekuwa yakifanyika kwa kutumia silaha mbalimbali zinazomilikiwa na wauaji, zikiwemo bunduki aina ya SMG. 
“Silaha zimezagaa hovyo huko, ni kama vile hakuna serikali katika eneo hilo huku watu wanaohusika na usalama wa raia wakiwa kimya,’’ alisema. 
Akihitimisha mwongozo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Wizara Maalumu) Mark Mwandosya, alisema haiwezekani mauaji hayo yaachwe yakiendelea. 
Alisema kazi ya serikali ni kulinda maisha ya wananchi wake na mali zao na si kuacha wananchi wake wanauana. 
Alisema hivi karibuni, Bunge litapokea taarifa ya tume teule, ambayo inachunguza matatizo ya migogoro ya ardhi, wafugaji na wakulima. 
Mwandosya alisema katika kujadili taarifa hiyo, suala hilo la Kiteto pia litajadiliwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru