NA THEODOS MGOMBA NA NJUMAI NGOTA
SERIKALI imewasilisha Bungeni muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi, ambao pamoja na mambo mengine, utaweka utaratibu wa kuwatangaza kwenye vyombo vya habari wakwepa kodi wote.
Akiwasilisha muswada huo bungeni jana, Waziri Fedha, Saada Mkuya Salum, alisema madhumuni ya muswada huo ni kuweka mfumo wa kisasa.
Waziri alisema nia ya kuwatangaza wakwepa kodi hao, ambao watathibitika kufanya hivyo, kutapunguza makosa sugu na ya makusudi.
Alisema mfumo huo wa kodi wa wazi, utahusisha kuhuisha ndani ya sheria moja vifungu mbalimbali vya sheria za kodi vinavyohusu usimamizi na utawala wa kodi.
Saada alisema mfumo uliopo sasa haujazingatia vigezo vya kimataifa, vinavyosisitiza kuwepo kwa sheria moja ya usimamizi na utawala wa kodi, ambayo inasimamia kodi zote.
Alisema kwa kupitisha sheria hiyo mpya, itasaidia kupunguza gharama za utawala, gharama za walipakodi kutimiza wajibu wao na kuepuka mianya ya rushwa.
Waziri alisema mambo mengine muhimu katika muswada huo ni pamoja na kuweka viwango vyenye uwiano sawa wa adhabu na faini kadri ya aina na ukubwa wa makosa ya kodi kwa kila aina ya kodi inayohusika.
Alisema muswada huo utaweka vifungu vya kuzuia ukwepaji kodi ndani ya sheria moja, badala ya kuwa na vifungu hivyo katika sheria ya kodi kama ilivyo katika utaratibu wa sasa.
Saada alisema kupitia muswada huo, watafanya marekebisho ya sheria za kodi husika kwa kuondoa vifungu vinavyohusiana na utawala na usimamizi.
Mjumbe wa kamati hiyo, Kidawa Hamid Salehe (Viti MaalumuñCCM), akisoma maoni ya kamati kuhusu muswada huo, alipongeza vifungu vya 93 hadi 99, ambavyo vinaruhusu mashauri ya kodi, ambapo kamishna mkuu anapewa mamlaka ya kufanya upekuzi, kukamata, kuchukua na kuuza mali za mlipa kodi kwa lengo la kukomboa kodi na kuzuia ukwepaji kodi.
Alisema sehemu hiyo inatoa mamlaka ya kutangaza kwenye vyombo vya habari wakwepa kodi sugu.
Kidawa alisema kamati imeona umuhimu wa kuwepo kwa kifungu cha 97, kinachomwezesha kamishna mkuu kuwatangaza wakwepa kodi sugu bila kujali hadhi zao.
Alisema kufanya hivyo kutakuwa fundisho kwa walipa kodi wote, ambao vitendo vyao huinyima serikali mapato na hivyo kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wananchi.
Kidawa alisema kamati hiyo inaona umuhimu wa kuwa na usimamizi wa kifungu hicho utaowezesha upatikanaji wa mapato stahiki kwa serikali.
Kwa mujibu wa Kidawa, kwa upande wa adhabu, muswada umeweka masharti mbalimbali yatakayotumika kupima ukubwa wa makosa ya kodi na kiwango stahiki cha adhabu.
ìKuhusu makosa mengine yatakayotendwa kutokana na kukiukwa kwa sheria hii, yataadhibiwa kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha muswada huu. Kifungu hiki pia kitahusika kutoa adhabu kwa yeyote atakayetoa siri kama zinavyoelezwa katika kifungu cha 21 cha muswada huu,îalisema.
Mjumbe huyo alisema kifungu cha 62(7), pia kimeboreshwa ili kutoweka ulazima wa mlipa kodi kuanza kudai kodi aliyolipa kwa ziada, badala yake, kamishna mkuu kuirudisha mara moja kodi hiyo iliyozidi bila kusubiri mlipa kodi kuomba kurejeshewa.
Alisema ili kutambua kwamba fedha hizo ni mali ya mlipa kodi, si sahihi kumtaka mlipa kodi kurejesha fedha hizo.
Kidawa alisema sehemu hiyo inabeba kifungu cha 70 hadi 74, ambacho kinabainisha masuala ya malipo na marejesho ya kodi yatafanywa chini ya mamlaka ya kamishna mkuu.
ìKifungu cha 71 kinaainisha taratibu zinazopasa kufuatwa wakati wa kuwasilisha maombi kwa ajili ya marejesho ya kodi kwamba yatafanyika kwa maandishi, yakionyesha ukokotoaji sahihi wa kodi husika, yakiambatana na ushahidi wa maandishi unaounga mkono maombi hayo,î alisema.
Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi-CCM), akichangia muswada huo, alisema ukipitishwa utaboresha makusanyo ya kodi na mapato ya serikali yataongeza na hivyo changamoto zinazolikabili taifa ni pamoja na kutokutekeleza baadhi ya miradi na kutegemea wahisani.
Alisema muswada huo umeweka utaratibu wa adhabu na kwamba adhabu kubwa aliyoiona ni ya kutangazwa katika vyombo vya habari kuwa hakulipa kodi.
ìKwa mtu mzima, kiongozi, mfanyabiashara mkubwa ambaye hataki biashara yake iingie doa, ambaye atataka benki zote zimuone ana thamani kubwa na anakopeshwa, hatataka kutangazwa katika vyombo vya habari, hili naliunga mkono,î alisema.
Mbunge huyo alisema utaratibu huo utakaowekwa, utekelezwe kwa sababu wakwepa kodi ni wafanyabiashara wakubwa, kwani wafanyabiashara wadogo hawajarasimishwa, kama wangeweka utaratibu rasmi, wangeweza kulipa kwani kodi yao ndogo.
Akizungumzia kuhusu matumizi ya TIN kwa walipa kodi, alisema jambo hilo ni zuri na kutoa maoni yake kwamba taarifa zilizoambatanishwa katika TIN ni chache, ikilinganishwa na taarifa za takwimu zilizopo kwenye vitambulisho vya taifa.
Akichangia muswada huo, Jitu Soni (Babati Vijijini-CCM), alisema ni mzuri ila ufanyiwe marekebisho kadhaa, kwani kwa kufanya hivyo, serikali itakusanya kodi kwa wingi zaidi.
Pia, aliiomba serikali itoe kipaumbele katika elimu ya mlipa kodi ili watu wengi waweze kulipa kodi ili nchi iweze kuwa na maendeleo makubwa.
Thursday, 13 November 2014
Wakwepa kodi sasa kuanikwa
07:11
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru