Thursday 13 November 2014

Uadilifu katika kodi kuipaisha nchi kiuchumi



NA WILLIAM SHECHAMBO
ENDAPO kila Mtanzania atalipa kodi kwa uadilifu na serikali ikitumia mapato hayo kama inavyostahili, Tanzania inaweza  kuingia kwenye kundi la nchi zenye uchumi wa kati kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja, imeelezwa.
Sababu nyingine, ambayo imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kasi ya kukua kwa uchumi wa Tanzania, ni uzalendo wa kununua bidhaa za nyumbani na kudai risiti.
Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati wa mahojiano maalum na kituo kimoja cha televisheni nchini.
Alisema Watanzania ndio watakaoitoa Tanzania ilipo sasa kiuchumi na kiupeleka hatua nyingine mbele, ambayo itaiwezesha nchi kujitegemea kwa asilimia zaidi ya 90 kwenye uandaaji wa bajeti ya mwaka wa fedha.
Mwigulu alisema kutokana na ukosefu wa uadilifu miongoni mwa Watanzania, hasa wenye kipato cha juu, nchi imeendelea kutegemea wahisani wa kimataifa katika utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo, hali inayosababisha kasi ya uchumi kuwa ndogo.
Alisema tatizo kubwa lililoko kwenye ukuzaji uchumi, ambalo serikali inaendelea na jitihada za kulitatua ni kuongezeka kwa tofauti kati ya wenye nacho na wasio nacho, ambapo wenye nacho ndio kundi linaloongoza kwa kukwepa kodi.

“Changamoto tuliyonayo ni tofauti kubwa iliyopo kati ya tajiri na masikini. Tunaendelea na mapambano ya kulipunguza hili pengo ili kila mwananchi awajibike kwa usawa wa stahili yake na kwa uadilifu wa hali ya juu,” alisema Mwigulu.

Aidha, alisema moja ya mikakati iliyopo ni kusimamia utoaji wa kodi kwa matajiri kwa kuziba mianya yote wanayoitumia kukwepa wajibu wa kulipa kodi na kisha kuyatumia mapato hayo kwa ajili ya kuwahudumia masikini.
Naibu waziri pia alisema kupitia matumizi sahihi ya mashine za EFD, serikali ina uhakika wa kupata zaidi ya asilimia 80 ya mapato yanayotokana na kodi, ambayo awali yalikuwa yanapotea kwa sababu tofauti.
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia umuhimu wa kudai stakabadhi kwa kila manunuzi wanayoyafanya, na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo, wameshiriki ukusanyaji wa kodi za mapato, ambazo ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kuhusu upotoshaji ulioko juu ya mabadiliko ya noti ya sh. 500 kuwa sarafu, Mwigulu alisema si kweli kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imefanya hivyo kutokana na mfumuko wa bei.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mzunguko mkubwa wa noti ya sh. 500, hali inayosababisha gharama kwa BoT za kuzalisha noti mpya kila mara, kwa idadi sawa ya noti nyingi za sh. 500 zilizoharibika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru